Na; Mwandisi wetu
Shahidi wa siri wa Jamhuri (P5) katika kesi Na.19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu ametoa ushahidi wake leo, Alhamisi Februari 12.2026, kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam
Akitoa ushahidi wake mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa yeye ana umri wa miaka 33, anaishi Kibangu -Ubungo, jijini Dar es Salaam akijishughulisha na Ujasiriamali/ machinga wa kuuza nguo na viatu kwa kutembeza maeneo mbalimbali ya Jiji hilo kama vile Mchikichini, Kariakoo, Posta ya Zamani, Feli na Posta Mpya, ambapo bidhaa hizo anachukulia Ilala Boma kabla ya kuanza kuzitembeza
Sambamba na hilo, shahidi huyo (P5) amesema wakati mwingine ili kuhakikisha ‘mkono unaenda kinywani’ amekuwa akijihusisha na uoshaji wa magari
Kuhusu kesi hiyo, P5 anasema Aprili 04.2025 akiwa amejipumzisha maeneo ya Posta ya Zamani Garden huku akiperuzi mitandao ya kijamii ya Facebook, Whatsapp na YouTube kupitia simu yake Smartphone Sonny ‘Galaxy’, aliona na kufungua video moja ndogo (kwenye mtandao wa Facebook) iliyokuwa ikimuonesha Tundu Lissu
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ajuwaye Nzengeli, P5 ameieleza Mahakama kuwa ili uweze kuingia kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook ni lazima kwanza uwe na account na internet ya kutosha, na yeye aliweza kuingia kwa sababu tayari alikuwa na vitu hivyo
Anasema Tundu Lissu anamfahamu kwa kumuona kwenye mitandao ya kijamii na Vyombo vya Habari, na kwamba anamjuwa kama mwanasiasa, na ndio maana alipoiona video hiyo alishawishika kuifungua ili kujuwa nini hasa amekizungumza
P5 ameieleza Mahakama kuwa, alipofungua video hiyo alimsikia na kumuona Lissu akisema kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 unaotumika kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais hautafanyika, na kwamba Lissu ‘aliapa’ kuwa atakinukisha, jambo lililoanza kumtia hofu
Ameendelea kueleza kuwa, pia alimsikia akisema kwamba Polisi wanatumika kuiba kura, na kwamba hata Majaji nao ni ‘Ma-CCM’ ndio maana hawatendi haki Mahakamani
Alipoulizwa na Wakili wa Serikali Mkuu Ajuwaye Nzengeli kuwa mzungumzaji alikuwa kwenye mazingira gani, P5 amejibu kuwa alimuona Lissu akiwa amesimama jukwaani, akiwa amevaa gwanda la Kaki, na T-shirt nyeusi kwa ndani, pia alivaa miwani na nyuma kulikuwa na pazia iliyokuwa imechagizwa na rangi za bendera ya Taifa
Baada ya kuona video hiyo, aliendelea kupumzika na kuperuzi mitandao mbalimbali kwa muda, lakini baadae aliondoka eneo hilo na kuelekea kwenye Kituo cha Daladala kwaajili ya kurudi nyumbani Kibangu -Ubungo, lakini alipofika Kituo cha Daladala Ubungo aliamua kuelekea ‘Maskani’ kwenye kijiwe cha Kahawa
Shahidi huyo ameendelea kueleza kuwa, alipofika kijiweni hapo alikuta mzozo kuhusu ile video ya Lissu aliyoiona awali akiwa Posta ya Zamani Garden, na kwamba wengi walionekana kumuunga mkono Lissu kwa hoja yake ya ‘kukinukisha’, na kwamba watu hao waliokuwa kwenye mzozo walieleza kuwa watahakikisha siku ya Uchaguzi watu hawaendi kupiga kura, na kupitia mzozo ule wasiwasi uliongezeka zaidi kwake akiona kwamba kuna kila dalili ya kutokea fujo siku ya Uchaguzi
Ameendelea kueleza kuwa, aliona wazi kuwa endapo hilo linalomtia hofu litatokea ni dhahiri amani itavurugika na kwamba wafanyabiashara wanaotembeza ‘kama yeye’ watashindwa kupata kipato na hivyo watapata njaa, hata hivyo baadae alitoka kijiweni hapo na kwenda moja kwa moja nyumbani, ambapo alimpigia simu mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Rama (Ndugu yake) akimuuliza kama amesikia habari zilizokuwa mtandaoni kuhusiana na Lissu
Anasema ndugu yake huyo anayefanya kazi ya Upolisi Tabata Relini alimjibu kuwa amelisikia na wanalifanyia kazi kikamilifu, na kwamba asiwe na wasiwasi wote
Shahidi huyo amesema, Aprili 09.2025 wakati anajiandaa kutoka nyumbani kwenye kwenye mihangaiko yake ya kila siku, alipigiwa simu na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Afisa wa Polisi, ambaye alimtaka afike Polisi Central, na kwamba alipofika akatakiwa kutoa maelezo kuhusu ile video ya Tundu Lissu aliyoiona Aprili 04.2025
Anasema akiwa Central Police alipelekwa kwenye chumba cha mahojiano, na baadae baada ya kukamilika kwa mahojiano hayo alirejea nyumbani
Hata hivyo, shahidi huyo wa siri wa Jamhuri (P5) anasema kile alichokitilia hofu ndicho kilichotokea siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.2025, kwani vurugu zilizotokea zilimpelekea yeye kukaa ndani karibu siku sita (6) bila kutoka nje, huku njaa ikimpiga,
Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Tundu Lissu alipata nafasi ya kumuuliza maswali ya dodoso (cross examination) akiainisha maeneo 12 aliyoona yana ‘utata’ wa maelezo ya shahidi, yaani utofauti uliopo baina ya maelezo ya shahidi aliyoeleza leo Mahakamani, na yale aliyoandika Polisi Aprili 09.2025
Maswali na hoja nyingi zilizoibuliwa na mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo, zilikosa majibu kutoka kwa shahidi huyo, na baada ya kumaliza maswali ya dodoso upande wa Jamhuri haukuwa na ziada juu ya shahidi husika
Kesi hiyo sasa imeahirishwa kwa muda hadi Saa 08:00 mchana, ambapo Jamhuri itamleta shahidi mwingine.