Latest Posts

RC MSENGI ATAKA UWAJIBIKAJI WA KWELI MTWARA, ASISITIZA USIMAMIZI WA MAPATO NA MIRADI

Mkuu mpya wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameweka msisitizo mkubwa kwenye uwajibikaji wa viongozi wa serikali za mitaa akitaka ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo usimamiwe kwa karibu ili kuhakikisha unaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Akizungumza Februari 12, 2026 katika hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika katika ukumbi wa Boma, Ofisi ya Mkoa wa Mtwara, Msengi amesema uwekezaji katika miradi pekee hautoshi bila usimamizi madhubuti wa utekelezaji wake na ubora wa huduma zinazotolewa.

Amesema ni wajibu wa watumishi wa umma na wadau wa maendeleo kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo ya Serikali, akionya dhidi ya urasimu unaoweza kuchelewesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Mbali na miradi, Msengi amegusia sekta za huduma za jamii akitaja elimu, afya na maji safi na salama kuwa ni maeneo yanayohitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali zinazotumika.

“Natambua kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa na iliyokamilika kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi. Tutaendelea kuisimamia ili iwe na tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa.” Amesema Msengi

Aidha, amerejea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayowataka watendaji kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao, kuimarisha uwajibikaji na kuyalinganisha na vipaumbele vya taifa, akisisitiza maadili na uadilifu kazini.

Katika eneo la ulinzi na usalama, Msengi amesisitiza umuhimu wa zoezi la uandikishaji wa wakazi na wageni, akiwataka viongozi wa mitaa na vitongoji kuhakikisha wanatambua watu wanaoingia na kutoka katika maeneo yao.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala katika hotuba yake ya kuaga amesema mkoa umeendelea kushuhudia mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani katika sekta za elimu, afya, miundombinu na uwekezaji na kueleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali na wananchi na kutoa wito wa kuendelezwa kwa ushirikiano huo chini ya uongozi mpya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!