Mganga Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dkt. Juma Mombokaleo, amewataka watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanatoa elimu ya kina kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya, ili kuongeza uelewa wa jamii juu ya faida na utaratibu wa mfumo huo.
Akizungumza wilayani Moshi, Dkt. Mombokaleo amesema kuwa elimu hiyo itasaidia kuondoa dhana potofu zilizopo miongoni mwa baadhi ya wananchi kuhusu uchangiaji na upatikanaji wa huduma kupitia bima ya afya.

Amefafanua kuwa bima ya afya ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu kwa wakati bila kukumbwa na changamoto ya gharama kubwa za papo kwa papo.
“Ni wajibu wetu sisi viongozi na watendaji kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwaeleza kwa lugha rahisi faida za kujiunga na bima ya afya pamoja na namna wanavyoweza kunufaika wao na familia zao,” amesema Dkt. Mombokaleo.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa watendaji katika utoaji wa elimu hiyo utaongeza idadi ya wananchi wanaojiunga na bima, hatua itakayochangia kuimarisha afya ya jamii na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa kaya zenye kipato cha chini.

Kwa mujibu wa Dkt. Mombokaleo, kiwango cha mchango wa shilingi 150,000 kwa mwaka kitamwezesha mnufaika pamoja na watoto au wategemezi wake wasiopungua watano kupata huduma za afya katika hospitali yoyote ndani ya Tanzania.
Ameongeza kuwa kifurushi hicho kinatoa jumla ya huduma 372, zikiwemo huduma za uchunguzi, matibabu ya magonjwa ya kawaida na sugu, pamoja na huduma za rufaa kulingana na taratibu za kitabibu.
“Kwa gharama hii, familia inakuwa na uhakika wa kupata huduma bila kulazimika kutoa fedha taslimu kila inapopata changamoto ya kiafya, hii ni hatua muhimu katika kulinda kipato cha kaya na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu kwa wakati,” amesisitiza.
Aidha, ameeleza kuwa wazee wasiojiweza, hususan wale wanaonufaika na mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), watalipiwa gharama za bima na Serikali ili kuhakikisha nao wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.