Latest Posts

MBUNGE SHAYO AWAPATIA VIJANA 30 WASIO NA UWEZO UFADHILI WA MASOMO VETA

Vijana Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wameshauriwa kutumia fursa ya elimu ya ufundi stadi kujijengea maisha bora ya baadae kwa kujiajiri na kumiliki ujuzi wao tofauti na kutegemea kuajiriwa pekee.

Ushauri huo umetolewa Februari 13,2026 na Mbunge wa Moshi Mjini Ibrahim Shayo maarufu Ibraline wakati akikabidhi vifaa vya shule kwa vijana 30 aliowafadhili kusoma katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kwa kipindi cha miaka mitatu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wakati wa kampeni.

“Nendeni mkasome, Taifa linahitaji wataalamu wabobezi katika nyanja mbalimbali nyie ni watu muhimu sana katika ujenzi wa nchi hii,” alisema Shayo.

Aliongeza kuwa ni furaha kwake kuona vijana hao 30 atakaowagharamia masomo kwa miaka mitatu wanamaliza kwa mafanikio wakijiajiri au kuajiriwa katika taasisi za umma na binafsi.

“Nitafurahi sana kusikia vijana niliowasomesha wote wamemaliza masomo yao na wanafanya kazi katika maeneo mbalimbali au kujiajiri, nendeni mkawe waaminifu na waadilifu, tambueni mnakwenda kusoma kwa ajili ya maisha yenu ya sasa na baadae” alisisitiza Shayo.

Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge, Samwel Kamandwa, alisema walipokea maombi 360 kutoka vijana wa kata 21 za Manispaa ya Moshi, na kisha kuendesha mchakato wa usaili kwa kuzingatia vigezo vya VETA.

“Baada ya kukamilisha mchakato wa uchambuzi, tulibaki na vijana 30 waliokidhi vigezo vya kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi,Mbunge atagharamia ada na michango yote inayotakiwa chuoni hapo kwa kipindi chote cha miaka mitatu,”Kamandwa.

Baadhi ya wanufaika wa ufadhili huo, akiwemo Debora Nko, George Mwita na Yusuph Mdee, walimshukuru Mbunge Shayo kwa msaada huo, wakisema bila ufadhili huo wasingeweza kuendelea na masomo kutokana na hali za kifamilia.

“Kwa kweli tusingeweza kusoma kutokana na uwezo mdogo wa familia zetu,tunakuahidi tutasoma kwa bidii na kufanya vizuri,” walisema.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!