Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa dharura likitaka makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza yawe ya kudumu, huku likionya dhidi ya hatua za Israel zinazoelekea kuitwaa kimabavu sehemu za Ukingo wa Magharibi.
Katibu Mkuu Msaidizi wa UN anayehusika na Masuala ya Kisiasa, Rosemary DiCarlo, ameeleza wasiwasi wake kuhusu mpango wa Israel wa kuongeza mamlaka ya kiraia katika maeneo yanayokaliwa. Amesema hatua hizo, zikitekelezwa, zitashusha vikwazo vya ukiritimba na kurahisisha unyakuzi wa ardhi na upanuzi wa makazi ya walowezi katika maeneo nyeti kama Hebron.
DiCarlo amebainisha kuwa Israel inazidi kubadilisha mazingira ya Ukingo wa Magharibi hatua kwa hatua, jambo ambalo linaathiri mamlaka ya ndani ya Palestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, amejibu kwa kuushutumu Umoja wa Mataifa kuwa una chuki dhidi ya taifa hilo na umepoteza mwelekeo.
Mkutano huu ulipangiwa kufanyika Alhamisi, lakini ukaahirishwa na kufanywa mapema ili kuepuka muingiliano wa ratiba na mkutano wa bodi uliotangazwa na Donald Trump, ambao ungetatiza usafiri wa wanadiplomasia wengi wanaohudhuria vikao vyote viwili.
DiCarlo amesisitiza kuwa kurahisisha vibali vya ujenzi kwa ajili ya Israel katika maeneo yanayojitawala na Wapalestina ni hatua ya hatari inayoweza kusababisha mivutano mipya na kuua matumaini ya suluhu ya mataifa mawili.