Latest Posts

ADAIWA KUMNYONGA MWENZAKE BAADA YA ALIYEKUWA MKEWE KUANZA UHUSIANO MPYA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mvuvi mmoja, Ndaishimiye Gerald Joseph (45), mkazi wa Kisiwa cha Zilagula, kwa tuhuma za kumuua mvuvi mwenzake, James Jastine Lameck (45), kufuatia wivu wa kimapenzi.

Tukio hilo la kikatili lilitokea alfajiri ya tarehe 19 Februari, 2026, majira ya saa 10:30 katika Kisiwa cha Zilagula, Kijiji cha Itabagumba, Wilaya ya Sengerema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, Februari 20, 2026, mtuhumiwa anadaiwa kumpiga marehemu ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumnyonga shingoni kwa kutumia mikono hadi kifo kilipomfika.

“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, baada ya aliyekuwa mke wa mtuhumiwa, Neema Mathias Lwasa, kutengana naye Februari 05, 2026 na kuanza uhusiano mpya na marehemu, ambapo walikuwa wakiishi pamoja katika makazi ya marehemu ndipo mtuhumiwa alipopata wivu na kwenda kutenda tukio hilo la kikatili”, imeeleza taarifa ya polisi.

Mwili wa marehemu James Jastine umeshafanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi. Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linaendelea kumhoji mtuhumiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa onyo kali kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi. Wamewasihi wananchi kutumia njia sahihi za kutatua migogoro ya kifamilia na kijamii, ikiwemo kuwashirikisha ndugu, viongozi wa dini, au kufuata taratibu za kisheria kupitia vyombo husika badala ya kutumia vurugu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!