Latest Posts

SAKATA LA MCHUNGAJI YANICK MBOMBO: POLISI DODOMA WASHANGAA TAARIFA ZA KUTEKWA KWAKE.

Jeshi la Polisi Tanzania limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa Mchungaji Yanick Mbombo Cele, wa kanisa la Ebenezer Restoration Ministry for all Nations, ametekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP David Misime, usiku wa Februari 22, 2026, Jeshi hilo limeeleza kushangazwa na taarifa hizo kwa kuwa mchungaji huyo, ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alishafukuzwa nchini baada ya kukamilisha hukumu ya makosa mbalimbali ya jinai.

Jeshi la Polisi limebainisha kuwa Mchungaji Mbombo alikamatwa Mei 15, 2025, mkoani Iringa kwa tuhuma nzito zilizojumuisha ubakaji na mauaji ya watoto ambapo alituhumiwa kuwashawishi wafuasi wake kuwabaka watoto na kukinga damu zao kwa ajili ya maombi.

Aidha alidaiwa kuwalipa watu wajifanye wagonjwa na walemavu kisha “waponywe” kanisani kwake ili kuvutia waumini na upekuzi nyumbani kwake ulibaini uwepo wa hirizi, pete za ajabu (magic faces), magamba ya konokono, na vitambaa vyenye damu.

Ingawa ushahidi wa mauaji haukutosheleza kumtia hatiani, Julai 14, 2025, Mbombo na wenzake walikiri makosa ya utapeli na kuendesha genge la uhalifu kupitia utaratibu wa plea bargaining. Walihukumiwa kulipa faini ya Shilingi milioni 20 na magari yao kutaifishwa. Baadaye, alikabidhiwa Idara ya Uhamiaji na kuondolewa nchini.

Msemaji wa Jeshi la Polisi amesema kuwa linaendelea na uchunguzi kubaini ukweli wa madai hayo ya kutekwa kwa mtu ambaye kimsingi hapaswi kuwepo nchini.

“Kutokana na hayo, Jeshi la Polisi limeshangaa kuona taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mchungaji huyo alikuwepo nchini na ametekwa na watu wasiojulikana. Hata hivyo, baada ya kuiona taarifa hiyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na linaomba kwa yeyote mwenye taarifa au ushuhuda utakaowezesha kuthibitisha taarifa hizo asisite kuziwasilisha kwenye kituo chochote cha Polisi kilicho karibu naye”, imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, saa chache kabla ya taarifa ya Polisi, kulikuwa na taarifa kupitia mitandao ya kijamii na kwa Baba Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula zikidai kuwa Mchungaji Mbombo alitekwa Jumatatu iliyopita akiwa nyumbani kwake Tabata, jijini Dar es Salaam.

Familia imedai kuwa watu wenye silaha waliokuwa kwenye gari aina ya Defender nyeupe walimchukua mbele ya watoto wake na dada wa kazi. Inadaiwa kuwa ndugu wamemtafuta vituo vyote vya polisi na uhamiaji bila mafanikio.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!