Kutokana na mkoa wa Njombe kufanya vizuri katika mitihani ya Darasa la Saba, Kidato cha Pili na Kidato cha nne Kitaifa, imeelezwa kuwa mafanikio hayo huanza na usimamizi ngazi za vijiji na kata kwa kufanya tathimini wenyewe kwenye mchakato wa kusimamia elimu jambo ambalo linasaidia kutoa matokeo chanya katika mkoa huo.
Kata ya Utalingolo iliyopo halmashauri ya mji wa Njombe ni miongoni mwa kata inayofanya vizuri kimkoa chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Erasto Mpete ambapo hii leo pia wamelazimika kufanya tathimini na kujadili nini kifanyike ili wapige hatua zaidi.
Pamoja na mambo mengine baadhi ya viongozi akiwemo Elia Chilatu ambaye ni Mtendaji wa kijiji cha Utalingolo wamesema wameweza kufikia hatua ya kuwachukulia hatua wazazi wasiopeleka watoto shuleni bila sababu za msingi.
“Wiki iliyopita tulibaini mtoto mmoja hajaripoti Magoda sekondari kwa hiyo baada ya kumuita mzazi hatua ya kwanza tulimuweka ndani masaa yasiyopungua matano na tukaazimia mtoto aende shuleni na ni kweli alitii na mtoto alienda sekondari”amesema Chilatu
Aidha Otilia Mahay ambaye ni afisa elimu kata pamoja na Erasto Mpete mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe ambaye pia ni diwani wa kata hiyo wamesema suala la elimu litaendelea kuwa kipaumbele huku wastani wa ufaulu kwa kila shule ndani ya kata ukiwa ni kuanzia 95% na kuendelea.