Latest Posts

TANZANIA NA ZAMBIA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia zimeeleza dhamira ya pamoja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na usalama ili kukabiliana na makosa yanayovuka mipaka, yakiwemo biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na magendo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Ally Gugu, Februari 23, 2026, wakati akifungua Mkutano wa nne wa Kamati ya Wataalamu wa Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama (JPCDS) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Arusha International Conference Centre (AICC) jijini Arusha,

Mhe. Gugu amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za kiusalama hususani matukio ya ugaidi, uhalifu wa kupangwa wa kimataifa na uhalifu wa mitandao.

Ameeleza kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Zambia umejengwa juu ya misingi imara iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo, na kwamba miradi ya kimkakati kama TanzaniaZambia Railway Authority (TAZARA) na TAZAMA Pipelines Limited ni vielelezo hai vya mshikamano na ushirikiano wa Kiafrika uliojengwa katika misingi ya kujitegemea.

Mhe. Gugu ameongeza kuwa kikao hicho kinatarajia kuibua mapendekezo thabiti yatakayowasilishwa katika ngazi ya Mawaziri kwa maamuzi zaidi.

Aidha, amewahakikishia dhamira ya dhati ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na Zambia katika maeneo yote kulingana na matishio ya kiusalama.

Mkutano huo wa Kamati ya Wataalamu unafanyika ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja ya Ulinzi na Usalama (JPCDS) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia utakaofanyika tarehe 27 Februari, 2026 jijini Arusha, ukiwa na lengo la kujadiliana na kuweka mikakati juu ya namna ya kushirikiana na kuongeza juhudi dhidi ya makosa yanayovuka mipaka.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!