Watanzania wamehimizwa na kukumbushwa wajibu wao mkubwa katika kuhakikisha kuwa tunu adhimu ya amani iliyopo nchini inaendelea kudumu kama nguzo kuu ya maendeleo yetu ya taifa na ustawi wa kila Mtanzania, ikielezwa kuwa bila ya amani na umoja hakuna maendeleo, demokrasia, wala ustawi wa kijamii unaoweza kupatikana.
Akizungumza kuhusu umuhimu amani, baadhi ya wananchi akiwemo Bw. Manase Zebedayo amesisitiza kuwa wazi kwamba amani ndio chachu ya uwekezaji, elimu bora, huduma bora za afya na ustawi wa wananchi wote, akibainisha kuwa mitandao ya kijamii na siasa za ushindani, tuziepuke na kuziogopa kauli za uchochezi, misimamo mikali ya kisiasa na mgawanyiko wa kijamii kwani ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuharibu misingi ya amani na utulivu nchini.
“Amani ni hali ya mtu kuwa na uhuru wa kufanya jambo lolote lile halali kisheria, amani tafsiri yake pia ni upendo pia, tunapopendana ndio amani yenyewe na kubwa zaidi tuendelee kushikamana, tudumishe hiki tulichonacho kwani sisi nchi yetu ni kisiwa cha amani.” Amesema Bw. Zebedayo.
Mwananchi huyu anaungana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa salamu zake za mwaka mpya ambapo pamoja na mambo mengine, Rais Samia aliwasihi Watanzania kutokubali tofauti za kiitikadi au kimtazamo kutokuwagawa na kuwapotezea malengo yao ya maendeleo na ustawi wa Taifa kwanj tofauti imekuwa ni sehemu ya demokrasia lakini tofauti hizo hazipaswi kuwagawa kwa namna yoyote ile.
Aidha katika salamu zake hizo, Rais Dkt. Samia alieleza kuwa Tanzania ni moja na wananchi wake wamejengwa na itikadi ya kuamini kuwa amani, umoja na mshikamano hujenga uzalendo na ndio virutubisho vinavyoiletea maendeleo endelevu na ustawi wa Watanzania.