Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwasi Kusini Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro amerejesha kiasi cha Shilingi milioni mbili laki sita na elfu hamsini (2,650,000) kilichotokana na mauzo ya viwanja vitano vya kijiji hicho, baada ya hatua za uchunguzi na ufuatiliaji zilizofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza na vyombo vya habari Machi 3,2026 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2025, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwa asilimia 10 ya mapato ya mauzo ya viwanja hivyo, sawa na Shilingi milioni mbili laki sita na elfu hamsini (2,650,000) haikuwekwa kwenye akaunti ya kijiji kama ilivyoamuliwa katika mkutano wa hadhara badala yake fedha hizo zilihifadhiwa nje ya mfumo rasmi wa utunzaji wa fedha za serikali.
Amesema kuwa baada ya kubaini hali hiyo, TAKUKURU ilimtaka mhusika kurejesha fedha zote na kuziingiza katika akaunti rasmi ya kijiji ambapo 28 Novemba, 2025, kiasi chote kilirejeshwa na kuwekwa katika akaunti ya Kijiji iliyopo NMB.
Katika hatua nyingine Kamanda huyo wa TAKUKURU amesema kuwa Taasisi hiyo ilifanikiwa kuokoa fedha za Serikali kiasi cha shilingi 9,621,430 katika miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kingondi na Kisangara pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya Msingi Kifaru Wilayani Mwanga baada ya Mzabuni kutumia vifaa visivyo na ubora uliokubalika kinyume na BOQ.
Kamanda Chaulo amesema hatua hiyo inaonesha umuhimu wa uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma na dhamira ya taasisi hiyo kuhakikisha mapato ya Serikali yanalindwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi.