Baadhi ya wajumbe wa kamati ya chakula katika Shule ya Msingi Likuyufusi iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wanadaiwa kuuza magunia 53 ya mahindi yaliyokuwa yamechangwa na wazazi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilman Kapenjama Ndile, alisema alifika shuleni hapo kufuatia kupokea malalamiko kutoka kwa wazazi waliokuwa wamechangia mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi.
Ameeleza kuwa jumla ya magunia 80 ya mahindi yalichangwa na wazazi, lakini kwa masikitiko makubwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya chakula ambao hawakuwa waaminifu waliuza magunia 53, hali iliyosababisha wanafunzi kukosa chakula shuleni.
Kutokana na tukio hilo, Wilman Kapenjama Ndile ametoa muda wa siku mbili kuhakikisha magunia 53 ya mahindi yanarejeshwa mara moja.
Aidha, ameagiza kufanyika kwa ukaguzi maalum ndani ya siku saba katika shule hiyo ili kufuatilia michango yote iliyokusanywa kwa ajili ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesema Mtendaji wa Mtaa wa Likuyufusi anashikiliwa na vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi, baada ya kushindwa kushughulikia kwa wakati changamoto ya upotevu wa magunia hayo ya mahindi katika Shule ya Msingi Likuyufusi.
Ndile amesisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya ubadhirifu vinavyohatarisha ustawi wa wanafunzi, na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.