Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema maendeleo ya kiuchumi hayawezi kupatikana bila amani na utulivu, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha analinda na kudumisha amani hiyo.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye futari iliyoandaliwa na Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es salaam.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira ya amani na mshikamano ambao umeifanya kuwa moja ya nchi zinazovutia wawekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo amewasisitiza wananchi kutumia kipindi cha mfungo kuliombea Taifa letu amani na mshikamano vizidi kutawala.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, katika kipindi cha mfungo, watu hufundishwa uwajibikaji na kuwa waaminifu jambo ambalo ni muhimu na linalopaswa kuonekana si wakati wa mfungo tu bali hata katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwa ujumla ili kujenga taasisi imara zenye kuaminika.

Mhe. Kikwete amesema, sekta ya bima na sekta ya fedha kwa ujumla zina nafasi muhimu sana katika maendeleo ya uchumi wa Taifa kwani bima ni chombo muhimu kinachosaidia kulinda mali, biashara na maisha ya wananchi dhidi ya hatari mbalimbali.
Amesisitiza kuwa, katika mazingira ya kisasa ya biashara na uwekezaji, hakuna uchumi unaoweza kukua bila kuwa na mfumo imara wa bima, Serikali inahitaji taasisi imara za kifedha zinazoweza kusaidia katika kusimamia hatari na kuhakikisha ustawi wa uchumi, wafanyabiashara wanahitaji uhakika wa kulindwa mitaji yao na wawekezaji wanahitaji mazingira salama ya kufanya biashara zao.