Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa mara ya kwanza imeanzisha programu ya kufuatilia masalia ya viuatilifu (pesticide residues) katika mazao yanayoingia kwenye masoko ya ndani, ikiwa ni jitihada za kulinda afya za walaji.
Katika hatua nyingine, TPHPA imefanikiwa kudhibiti viuatilifu visivyokidhi ubora vyenye jumla ya lita 435,390 na kuvirejesha katika nchi vilikozalishwa kwa kipindi cha mwaka 2024/2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti matumizi ya viuatilifu hatarishi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Machi 24,2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Profesa Joseph Ndunguru, wakati akizungumzia mafanikio ya TPHPA katika kipindi cha miaka mitatu.

Amesema kuwa hadi sasa utekelezaji wa programu hiyo umekamilika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, huku zoezi la uchukuaji wa sampuli likiendelea katika mikoa mingine.
Akizungumzia matarajio ya serikali kufuatia kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, Profesa Ndunguru amesema kuwa ni pamoja na kuongeza uhakika wa chakula na malighafi za viwandani kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Ameongeza kuwa serikali pia inalenga kuongeza ufanisi katika shughuli za afya ya mimea na udhibiti wa viuatilifu kupitia matumizi bora ya miundombinu, rasilimali watu na vitendea kazi.

“Tunatarajia kuongezeka kwa mapato ya serikali pamoja na kupungua kwa madhara ya kiafya kwa binadamu yanayotokana na masalia ya viuatilifu, sumu kuvu, madini mazito (heavy metals) na visibika vingine kwenye mazao,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa serikali kupitia TPHPA inatarajia kupunguza uwepo wa viuatilifu bandia sokoni kutokana na kuimarishwa kwa udhibiti katika utengenezaji, uingizaji, usambazaji na uuzaji. Pia alieleza kuwa juhudi hizo zitasaidia kupunguza uvamizi wa visumbufu vipya kupitia kuimarishwa kwa uchunguzi wa visumbufu (pest surveillance).
Kuhusu vipaumbele, Profesa Ndunguru amesema mamlaka hiyo itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu na watumishi wake, ambapo jumla ya shilingi bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia 2026 hadi 2031.