Latest Posts

MIRADI YA MAKAZI YA TBA YATAJWA KUWA KICHOCHEO CHA UCHUMI; KAMATI YA PIC YAPONGEZA MATUMIZI YA MAPATO YA NDANI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Masanja Kadogosa, amesema uwekezaji wa makazi unaotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) una mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi, kutokana na thamani ya miradi hiyo pamoja na uwezo wake wa kuongeza ajira.

Kadogosa ametoa kauli hiyo leo, tarehe 24 Machi 2026, jijini Dar es Salaam, wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua miradi ya makazi inayotekelezwa na TBA, ambapo amesema miradi hiyo imeendelea kuchochea mzunguko wa fedha katika sekta ya ujenzi kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wakandarasi, mafundi na wasambazaji wa vifaa.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo pia unaongeza thamani ya mali za umma na kuchochea maendeleo ya miji, jambo linaloimarisha mazingira ya makazi na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Charles Msonde, amesema matumizi ya mapato ya ndani ya TBA katika utekelezaji wa miradi hiyo yanaonesha uwezo wa taasisi za umma kujitegemea kifedha na kuwekeza kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inapunguza utegemezi wa bajeti kuu ya serikali na kuwezesha miradi kutekelezwa kwa wakati huku ikitoa manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia ajira na huduma bora za makazi.

Aidha, ameongeza kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati ya kupanua uwekezaji huo kupitia ubia na sekta binafsi (PPP), hatua itakayosaidia kuongeza mtaji wa miradi, kuharakisha utekelezaji wake na kuchochea zaidi ukuaji wa sekta ya ujenzi pamoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!