Latest Posts

MAGEREZA: TUNDU LISSU YUKO SALAMA NA AFYA YAKE NI NJEMA

Jeshi la Magereza nchini Tanzania limetoa kanusho kali dhidi ya taarifa zilizochapishwa na baadhi ya magazeti leo, zikidai kuwa hali ya afya ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ni mbaya na inatia shaka.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Jumatano, Machi 25, 2026, jijini Dodoma, Msemaji wa Jeshi la Magereza, SACP Elizabeth G. Mbezi, amesisitiza kuwa taarifa hizo siyo sahihi na zimelenga kuleta taharuki isiyo na msingi katika jamii.

“Kimsingi taarifa hiyo siyo sahihi ni ya kuupuzwa kwani ina lengo la kuleta taharuki katika jamii. Jeshi linapenda kuujulisha umma kuwa ndugu Tundu Lissu yuko salama na afya yake ni njema”, imeeleza taarifa hiyo

SACP Mbezi ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kufuata misingi ya taaluma yao, ikiwemo kuhakiki taarifa kutoka kwenye vyanzo sahihi kabla ya kuzisambaza kwa umma. Amesema Jeshi hilo linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu huku likithamini utu na haki za binadamu kwa wafungwa na mahabusu wote.

Taarifa hii inakuja siku kadhaa baada Lissu kuieleza Mahakama ya Rufani yuko katika hatari ya afya yake kuathirika zaidi kwa kushindwa kuhudhuria kliniki ya matibabu yake kutokana na kushikiliwa mahabusu kwa muda mrefu.

Aliiomba Mahakama hiyo kulisikiliza kwa dharura shauri la mapitio lililofunguliwa mahakamani hapo na Jamhuri dhidi yake kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kuikatalia kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi ya uhaini inayomkabili, ambalo limesababisha usikilizwaji wa kesi hiyo kusimama kwa muda usiojulikana.

Alidai kama shauri hilo lisiposikilizwa na kuamuliwa haraka basi hali ya afya yake itazidi kuathirika kwa kuzidi kukosa huduma hizo za kiafya kutokana na kuendelea kushikiliwa mahabusu, hivyo kupata madhara ambayo hayataweza kurekebishika na kukwamisha haki kutendeka.

Lissu alielezea hofu yake hiyo ya kuathirika kwa kukosa huduma za kiafya wakati alipowasilisha majibu yake ya maandishi dhidi ya hoja za Jamhuri katika shauri hilo la mapitio.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!