Latest Posts

ALIYEMUUA M/KITI WA KITONGOJI NA KUONDOKA NA KICHWA CHAKE AKAMATWA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mtu aitwaye Reginald Prosper Riwa (33) kwa tuhuma za mauaji ya Ezekiel Edward Temu (62), aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masaela, Kata ya Kilema Kusini, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Akieleza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa, amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 24, 2026, majira ya saa tatu asubuhi katika Kitongoji cha Masaela. Inadaiwa kuwa mtuhumiwa Reginald Prosper Riwa, mkazi wa kijiji hicho, alimvamia na kuanza kumkimbiza Ezekiel Edward Temu na kumpata, kisha kumkata kwa kutumia kitu chenye makali shingoni na kutenganisha kichwa na kiwiliwili, kisha kuondoka na kichwa hicho akiwa amekining’iniza.

Kamanda Maigwa amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni matatizo ya afya ya akili ya mtuhumiwa, ambaye aliwahi kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

“Mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa mahojiano, na atafikishwa mahakamani baada ya kukamilisha taratibu za kiuchunguzi na upelelezi,” amesema Kamanda Maigwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!