Latest Posts

WAMILIKI WA VITUO VYA MAFUTA WAKAOHODHI MAFUTA ILI WAUZE BEI KUBWA WAONYWA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amesema serikali itawachukulia hatua za kisheria wamiliki wa vituo vya mafuta watakaojihusisha na kununua mafuta kwa wingi kwa lengo la kuyahifadhi na baadaye kuuza kwa bei kubwa.

Dkt Mataragio ametoa kauli hiyo Machi 25 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kutembelea tanki la kuhifadhia mafuta la kampuni ya Camel Oil jijini Dar es Salaam, Dkt. Mataragio amesisitiza kuwa serikali imeanza kubaini dalili za baadhi ya wafanyabiashara kufanya biashara kinyume na utaratibu wa kawaida, hali inayoweza kusababisha uhaba bandia wa mafuta nchini.

“Serikali haitavumilia vitendo hivyo na hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika, na pia hakuna sababu ya wananchi wala wafanyabiashara kuwa na hofu kuhusu upatikanaji wa mafuta na kuanza kununua mafua kwa wingi ili mengi waweke kuhifadhi”, amesema Dkt Mataragio

Amefafanua kuwa serikali imejipanga kikamilifu kukabiliana na changamoto zozote, ikiwemo athari za vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, na kuongeza kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta itakayoweza kudumu hadi mwezi Julai mwaka huu.

Amesema ziara hiyo imelenga kujiridhisha na hali halisi ya upatikanaji wa mafuta pamoja na mwenendo wa usambazaji wake nchini, na kwamba ameridhishwa na kiwango cha akiba kilichopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andelile, amesema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha usambazaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika nchini kote.

Dkt. Andelile ameeleza kuwa pamoja na changamoto za soko la dunia hususan kutokana na vita Mashariki ya Kati, bado hakuna upungufu wa mafuta nchini, huku akionya kuwa tabia ya kununua mafuta kwa wingi kupita kiasi inaweza kuleta taharuki na kuathiri mfumo wa usambazaji.

Aidha, ameongeza kuwa ongezeko la gharama za uagizaji mafuta ikiwemo usafirishaji, bima na ununuzi kwa fedha za kigeni linaweza kuathiri bei za ndani, lakini serikali inaendelea kufanya tathmini kuhakikisha bei zinabaki kuwa himilivu kwa wananchi.

Naye Meneja Mkuu wa Camel Oil, Saleh Bajber, amesema kampuni hiyo ina akiba ya kutosha ya mafuta na inaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana kwa uhakika, huku akiwataka wafanyabiashara kuzingatia utaratibu wa kawaida wa biashara.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!