Latest Posts

AIRTEL AFRICA YAPUNGUZA MATUMIZI YA DIZELI KWA LITA MILIONI 9.1

LUSAKA, ZAMBIA: Airtel Africa Plc imetangaza kuwa imefanikiwa kuokoa lita milioni 9.1 za mafuta ya dizeli katika mwaka wake wa fedha wa 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza biashara endelevu na kupunguza athari za shughuli zake kwa mazingira.

Mafanikio hayo yametokana na juhudi za kampuni kupunguza utegemezi wa mafuta ya dizeli kwa kuongeza matumizi ya nishati mbadala. Katika kipindi hicho, Airtel Africa ilihamishia minara 390 kutumia umeme wa gridi ya taifa, hatua iliyoongeza ufanisi wa matumizi ya nishati na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa Ripoti ya Tathmini ya Uendelevu (Sustainability Scorecard) jijini Lusaka, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema kampuni inaendelea kujenga Afrika endelevu, jumuishi na yenye mawasiliano ya uhakika kupitia uwekezaji unaozingatia mazingira na maendeleo ya jamii.

Ripoti hiyo pia inaonyesha Airtel Africa ilirejeleza asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo wa uchumi rejeshi (circular economy). Kwa mujibu wa Taldar, uendelevu wa mazingira ni nguzo muhimu ya mkakati wa kampuni katika kupanua huduma na fursa kwa mamilioni ya Waafrika.

Katika huduma za kifedha, Airtel Money sasa inahudumia wateja milioni 54.1 kupitia mawakala milioni 2.4, huku asilimia 44.1 ya wateja wake wakiwa wanawake, hatua inayochangia kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia huduma za kifedha za kidijitali.

Kupitia Airtel Africa Foundation, kampuni imewekeza dola za Marekani milioni 6.2 katika miradi ya ujumuishi wa kifedha, elimu, mazingira na ujumuishi wa kidijitali. Aidha, kwa kushirikiana na UNICEF, imeunganisha shule 3,296 na intaneti ya bure, kunufaisha zaidi ya wanafunzi milioni mbili na walimu 38,868.

Zaidi ya vijana 30,000 wamepata mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kupitia programu mbalimbali za kampuni, huku wanafunzi zaidi ya 250 wakinufaika na ufadhili wa masomo ya shahada katika fani za STEM kupitia Airtel Africa Tech Fellowship.

Airtel Africa kwa sasa inatoa huduma katika nchi 14 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuhudumia zaidi ya wateja milioni 183.5, ikiendelea kuwekeza katika ujumuishi wa kidijitali na kifedha pamoja na maendeleo endelevu ya bara la Afrika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!