Kukuza vipaji vya soka kwa vijana mkoani Geita kumeendelea kushika kasi kupitia Kituo cha Michezo cha Jaspers, ambacho kimeanza rasmi msimu wa pili wa mashindano ya Jaspers Day, yakilenga kuwapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao, kujifunza ushindani wa kimichezo na kujitangaza mbele ya wadau mbalimbali wa soka.
Mashindano hayo yamezikutanisha timu na vituo mbalimbali vya michezo kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Geita, hatua inayotajwa kuongeza mshikamano, kukuza ushindani wa kirafiki na kutoa burudani kwa jamii.
Msimu wa pili wa Ligi ya Jaspers Day umefunguliwa rasmi kwa mchezo uliowakutanisha Masenari FC na Jaspers FC, huku viongozi wa kituo hicho wakieleza kuwa maandalizi yamekamilika na matarajio ni kuona vijana wengi zaidi wakinufaika kupitia mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ligi hiyo, Katibu Mkuu wa Kituo cha Michezo cha Jaspers, Shaneti Martine, amesema mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kuendelea kuibua vipaji vya vijana na kuwapa nafasi ya kuonekana mbele ya makocha, wadau na vilabu vinavyoweza kuviendeleza.
Katibu wa Mkuu wa cha cha Mpira Wilaya ya Geita Shafii Mwinyimvua ameelezea dhamira yao kama chama ni kuona wanaendelea kuwaunga wadau mbalimbali ambao wanafanya mashindano Wilayani humo.
Ligi hiyo imedhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya YAS, ambapo Meneja wa YAS Mkoa wa Geita, Willington Byekwaso, amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na Jaspers kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya michezo na kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao kupitia soka.

Wakati mashindano hayo yakianza, timu ya Mkapa FC nayo ilitumia fursa hiyo kuzindua rasmi jezi mpya pamoja na mpira watakaoutumia katika msimu huu wa Ligi ya Jaspers Day, huku uzinduzi huo ukipambwa na shamrashamra mbalimbali zilizovutia mashabiki waliojitokeza kushuhudia ufunguzi wa michuano hiyo.
Mashindano ya Jaspers Day yanatarajiwa kuendelea kwa wiki kadhaa yakishirikisha timu mbalimbali za vijana, huku yakitarajiwa kuwa chachu ya kuibua vipaji vipya vitakavyoweza kufikia ngazi za juu za soka nchini.