Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Madini na Tume ya Madini nchini kusimamia wachimbaji wadogo waliopata leseni na wakawekeza mitaji yao wasinyang’anywe maeneo kwa kisingizio walipewa maeneo ya wachimbaji wakubwa.
Amesema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Madini mwaka 2024 yaliyoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) akiongeza kwamba ni jambo lisiloeleweka mamlaka kumpatia mtu leseni na baada ya kuwekeza ananyang’anywa leseni na yuleyule aliyempa leseni.
Dkt. Mpango amesema Serikali imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kurasimisha maeneo yenye milipuko ya madini (rush).
“Nimeambiwa kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Tume ya Madini ilitoa Leseni za Uchimbaji Mdogo (PMLs) 6,934, Biashara (BLs)1,616 na Leseni za Uchenjuaji wa Madini (PCLs) 35. Ongezeko hilo la utoaji wa leseni ni matokeo ya uhamasishaji wa uwekezaji uliofanywa katika Sekta ya Madini” Amesema Dkt. Mpango.
Ametumia fursa hiyo kuwasihi wachimbaji wote, waongezaji thamani na wafanyabiashara wa madini kuendelea kufuata sheria ili kuepuka usumbufu ikiwamo kufutiwa leseni za madini.
“Nimeelezwa pia kuwa, wachimbaji wadogo wana malalamiko kuhusu tozo mbalimbali zinazotozwa na halmashauri mbalimbali. Nawaomba halmashauri zote za wilaya na miji, ziandae sheria ndogondogo (by-laws) ambazo hazikinzani na Sheria ya Madini ili kuona namna bora ya kuweka tozo hizo” Ameeleza Dkt. Mpango.
Aidha, ametoa rai kwa halmashauri zote zenye migodi kutumia fursa za uwepo wa migodi katika maeneo yao kwa kuyatumia mapato yanayopatikana kama chachu ya kuleta maendeleo yenye tija kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
“Nashauri Halmashauri kuendelea kuwa wabunifu katika kubuni miradi hasa inayowawezesha wananchi katika kujipatia kipato ili kuongeza mzunguko wa fedha na kuleta maendeleo endelevu kwa kuwa rasilimali madini kuna siku zitakwisha” Ameongeza Dkt. Mpango.
Akiwa katika banda la maonesho la benki ya NMB Mkuu wa Idara ya Biashara wa benki hiyo Alex Mgeni amesema NMB imekwishatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 43 kwa wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na FEMATA huku ikiendelea kuboresha huduma zake na kutoa elimu kwa wachimbaji hao ili kujua umuhimu wa utunzaji wa fedha na mazingira.
Awali Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina aliishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa inaowapa wachimbaji wadogo tofauti na ilivyo kwa mataifa mengine.