Latest Posts

GLOBAL EDUCATION LINK YADAHILI WANAFUNZI MAONESHO YA VYUO VIKUU ZANZIBAR

Wakala wa Elimu ya Vyuo Vikuu nje ya Nchi Global Education Link (GEL), imeanza udahili wa papo hapo wa wanafunzi kwenye maonesho yanayoendelea kwenye viwanja vya Maisala visiwani Zanzibar.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa GEL, Abdulimalick Mollel wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho hayo yanayoendelea visiwani humo.
 
Amesema kwenye maonesho hayo kuna vyuo vya nje ya nchi ambavyo vimetoa udhamini wa asilimia 50 kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma kwenye vyuo hivyo na vingine vimetoa ufadhili wa asilimia 100.
 
“Tumeleta wawakilishi wa vyuo 20 kutoka Iran kuna ufadhili wa asilimia 100 analipiwa kila kitu na kuna vyuo ambavyo mwanafunzi atalipiwa asilimia 50 ya ada, kwa hiyo mwanafunzi akija kwenye maonesho haya akichagua kozi GEL tunamdahili hapahapa,” amesema Mollel.
 
Aidha amesema manufaa mengine ya maonesho hayo ni uhusiano wa vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi kwani uzoefu unaonesha kuwa asilimia kubwa ya wahitimu wa vyuo vya nje ya nchi wanaajiriwa mara tu wanapomaliza vyuo.
 
Amesema mara nyingi wanafunzi wanaohitimu vyuo vya hapa nchini huanza kuhangaika kutafuta ajira kwenye maeneo mbalimbali na kulalamikia ugumu wa ajira wakati vyuo vya nje hali ni tofauti kwa wahitimu wao.
 
“Vyuo vya nje vinafanikiwa kutoa wahitimu ambao wanaajiriwa mara tu wanapohitimu ndiyo maana tumewakutanisha na vyuo vya ndani ili waweze kubadilishana maarifa, wao wanafanyaje kuwaaandaa wanafunzi tunaangalia je ni suala la mitaala au ushirikiano mwema na taasisi za ajira, Kwa hiyo tulicholeta hapa ni ushirikiano baina ya vyuo hivi kama kuna chuo kikuu cha hapa ndani kilichoko tayari kushirikiana na chuo chochote cha nje watakutana na kubadilishana ujuzi na maarifa mbalimbali ili waweze kutoa wahitimu bora,” Amesema Mollel.
 
Fursa nyingine iliyoelezwa na Mollel ni kupata udahili kwani baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikosa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu kutokana na ufinyu wa nafasi kwenye baadhi ya kozi wanazoomba hasa zile za afya na uhandisi.
 
Amesema idadi ya wanafunzi wanaoomba nafasi za kozi za afya na uhandisi ni wengi kuliko nafasi zilizopo hivyo kuna umuhimu wa kuwatafutia nafasi kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi.
 
“Tumekuja na vyuo hapa ambavyo vinaruhusu wanafunzi kudahiliwa hapa nchini akasoma kwenye chuo cha nje kwa miaka kadhaa kisha akarudi kumalizia elimu yake hapa Tanzania kwa hiyo sisi tunaona hii ni fursa kwa vijana wetu,” Amesema Mollel.
 
Aidha ametoa wito kwa wanafunzi wa Zanzibar na wadau wa elimu kuwa dunia imekuwa kama kijiji hivyo wanatakiwa kutumia fursa za nje kwani hata gharama za masomo za vyuo hivyo zinalingana na za masomo ya hapa nchini.
 
“Watanzania wachangamkie fursa za ufadhili wa vyuo vikuu wasidharau kwasababu tuna mtindo wa wa kudharau kwa sababu ya kuogopa kujaza fomu zenye maelezo mengi lakini sisi tuna ofisi hapa Zanzibar waje tutawatafsiria maelezo hayo, unaweza kukuta fomu moja ya ufadhili ina karatasi hadi 13 sasa, kwa mwanafunzi ni mara yake ya kwanza kuomba ufadhili anakata tamaa lakini kwa kuwa tuko hapa waje tuwaelekeze na tuko hapa kufungua fursa zilizoko duniani ili wanafunzi waweze kusoma nje,” amesema Mollel
 
Mwisho ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na Global Education Link kuendelea kuwatafutia fursa za elimu ya juu nje ya nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!