Taasisi ya Abilis Foundation, kwa kushirikiana na Foundation for Disabilities Hope (FDH), imeendesha mafunzo ya siku moja jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi wa FDH kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana Wenye Ulemavu katika Uongozi kwa ajili ya kukuza demokrasia nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwezeshaji kutoka Abilisi Foundation, Yasin Shehaghilo, alieleza kuwa mradi huo unalenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake na wasichana wenye ulemavu katika chaguzi zijazo, ikiwemo kugombea nafasi za uongozi. Taasisi ya FDH imepokea ruzuku kutoka Abilisi Foundation kwa ajili ya kusaidia jamii kupitia mradi huu.
Mradi huo utaanza kutekelezwa katika kata tatu za Wilaya ya Kondoa, ambazo ni Kilimani, Chemchem, na Borisa, pamoja na kata ya Mpunguzi mjini Dodoma. Mafunzo haya yamefanyika katika ofisi za FDH zilizopo Ipagala Ilazo West, na yanatarajiwa kuwa kichocheo cha elimu na uelewa wa masuala ya uongozi na haki za watu wenye ulemavu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.
Shehaghilo alifafanua kuwa Abilisi Foundation, taasisi yenye makao yake Arusha lakini inayotoka nchini Finland, tayari imefadhili zaidi ya vikundi na taasisi 10 za watu wenye mahitaji maalum. Ruzuku hii inalenga kuwapa wanawake na wasichana wenye ulemavu nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kisiasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, alitoa shukrani kwa Abilisi Foundation kwa kuwapatia ruzuku hiyo. Alisema mradi huo utaimarisha uwezo wa wanawake na wasichana wenye ulemavu kushiriki katika chaguzi na kuchukua nafasi za uongozi ili kuendeleza ajenda za watu wenye ulemavu.
“Jamii ya watu wenye ulemavu inapaswa kuelimika, kuchangamkia fursa zilizopo, na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika suluhisho la changamoto zinazowakabili,” amesema Salali.
Mradi huu, unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Novemba 2024 hadi Novemba 2025, utahusisha utoaji wa mafunzo kwa wanawake na wasichana wenye ulemavu pamoja na kubadilishana mbinu za kushughulikia changamoto zinazowakabili katika jamii.
Salali alisisitiza dhamira ya FDH kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo chanya kwa watu wenye ulemavu, huku akiahidi ushirikiano wa karibu kati ya FDH na Abilisi Foundation kufanikisha malengo yao ya pamoja.