Latest Posts

ACHENI SIASA ZA MALUMBANO HAZILETI MAENDELEO- DKT. BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa jimbo hilo kuacha siasa za malumbano kwani hazileti maendeleo na badala yake wajikite katika kujiletea maendeleo.

Dkt. Biteko ameyasema hayo wilayani Bukombe Mkoa wa Geita wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bukombe kwa mwaliko wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita katika mkutano uliolenga  kutathmini hali ya maendeleo kwenye jimbo hilo.

Dkt. Biteko amesema Wanabukombe hawana mtu mwingine wa kuwaletea maendeleo isipokuwa wao wenyewe na kuongeza kuwa siasa za malumbano hazileti maendeleo bali zinayachelewesha hivyo amewasisitiza  wananchi hao kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, kuhusu uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa jimbo hilo kuchagua viongozi wanaofaa  na wanaotokana na CCM  ili kutocheleweshewa maendeleo na kuwaasa kuwa wajifunze kuushinda ubaya kwa wema.

Akizungumzia miradi ya maendeleo jimboni Bukombe Dkt. Biteko amempongeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutosha takribani Shilingi bilioni 79 katika mwaka mmoja kwa ajili ya maendeleo Wilaya ya Bukombe kwenye sekta ya elimu, afya pamoja na  miradi mingine ya maendeleo.

Ameongeza kuwa mwaka 2015 Wilaya ya  Bukombe ilikuwa na vituo vya afya viwili na zahanati 4, mtandao wa barabara ulikuwa kilomita 256 , mtandao wa maji wilaya nzima ulikuwa chini ya asilimia 15  na  hakukuwa na  sekondari kwenye kata, lakini sasa kuna shule mpya za sekondari 7, shule za msingi mpya 11, vituo vya kutolea huduma za afya 25 na mtandao wa barabara umefikia kilomita 1400 hivyo amewataka wananchi kutembea kifua mbele  kwa maendeleo yaliyopo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais- TAMISEMI,  Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka matokeo zaidi kuliko maneno na ndiyo maana ameagiza TAMISEMI kuhakikisha inakarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua, na kuhakikisha watumishi wa sekta ya afya na walimu wanapelekwa wilayani Bukombe kwa maslahi mapana ya wananchi pamoja na  kuboresha maendeleo.

“Wananchi wa Bukombe mna bahati ya kuwa na kiongozi mchapakazi, mpenda maendeleo na mwenye kiu ya kuleta maendeleo hivyo mumuenzi kwa vitendo’.” Amesema Dugange.

Mkutano huo wa hadhara ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella, Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Geita, Rose Busiga na Wenyeviti wa CCM Mkoa na Wilaya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!