Chama cha ACT Wazalendo kimepinga vikali kufungiwa kwa maudhui ya mtandaoni ya kampuni ya Mwananchi Communication Limited hivyo kutoa wito kwa serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuondoa zuio hilo ili MCL iendelee kuchapisha maudhui ya mtandaoni kama ilivyokuwa awali
“Tumesikitishwa na tunalaani taarifa ya TCRA ya Oktoba 02.2024 kusitisha leseni ya huduma za maudhui mtandaoni kwa lampuni ya Mwananchi Communication Limited inayojumuisha Mwananchi Digital, The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti kwa siku 30”
Taarifa kwa umma ya chama hicho iliyotolewa leo, Alhamisi Septemba 03.2024 imeeleza kuwa chama hicho kinalaani kwa kuwa taarifa hiyo ni tishio na inaashiria kuendeleza mazingira kandamizi kwa vyombo vya habari nchini ili visifanye kazi zao kwa uhuru kupitia vifungu kandamizi vinavyotumiwa kuzima huru huo
Aidha, taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Rahma A. Mwita ambaye ni Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ACT Wazalendo imefafanua kuwa kampuni ya Mwananchi Communication Limited ilichapisha video ya katuni inayoonesha hofu za wananchi kuhusu matukio ya utekaji, kupotea na kuuawa kwa wananchi bila ya vyombo vya dola kuchukua hatua stahiki
ACT Wazalendo inadai kuwa kufungiwa kwa kampuni ya Mwananchi Communication Limited kuchapisha maudhui ya mtandaoni ambayo ni sehemu ya kazi yake ni muendelezo wa serikali ya kuzuia na kuvidhibiti vyombo vya habari kufanya kazi kwa weledi nchini
“Serikali inajaribu kuviziba mdomo vyombo vya habari vinavyoeleza changamoto halisi za Watanzania na kujaribu kuvitaka vibadili uelekeo wa kuhabarisha ili viingie kwenye uelekeo wa kutoa habari zinazoifurahisha serikali pekee, jambo ambalo ni hatari sana, matukio ya kukamatwa kwa waandishi wa habari, kuzuia kwa vyombo vya habari na hili la kufungiwa kwa maudhui ya mtandaoni ya kampuni ya Mwananchi Communication Limited inaonesha bado uhuru wa habari haujaimarika na hautabiriki licha ya mahubiri ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan”