Chama cha ACT Wazalendo, na hata Kiongozi wa Chama hicho yeye binafsi Dorothy Semu kimeeleza kuwa kimekuwa kikifuatilia na kutafakari kwa undani hali inayoendelea nchini na hasa kuhusiana na matukio yanayoripotiwa ya utekaji na mauaji kwa upande mmoja na hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kuitisha maandamano Jumatatu ya Septemba 23 2024 kwa upande mwingine
Chama hicho kimesema kwa jinsi hali inavyoendelea hapa nchini kwa sasa ishuhudiwa kila upande kati ya CHADEMA na Serikali na vyombo vya ulinzi na hususani Jeshi la Polisi wakishikilia misimamo yao waliyoitoa siku za nyuma
Taarifa ya chama cha ACT Wazalendo iliyotolewa leo, Jumapili Septemba 22.2024 iliyosainiwa na Kiongozi wa chama hicho Dorothy Semu imeeleza kuwa, bada ya kutafakari kwa kina ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Uongozi ya Taifa ya imetoa wito ufuatao;-
(I) Kwamba kila mtu anatambua na kuona kuwa nchi yetu (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) imeingia kwenye mvutano kutokana na matukio ya karibuni, mvutano ambao hauna afya kwa mustakbali wa umoja wetu, amani yetu, haki na demokrasia yetu
(II) Kwamba mvutano huo umepelekea kila upande unaohusika kukaza kamba na kutetea msimamo wake, hali ambayo haitoi nafasi ya vichwa kutulia na kutafuta suluhisho muafaka na la kiuongozi litakalotutoa hapa tulipo
(III) Kwamba inawezekana pande zote mbili zina hoja za msingi katika hoja na misimamo yao lakini tatizo kubwa ni kuwa hawajapata fursa ya kufanya mawasiliano yanayostahiki kwa maslahi mapana ya Taifa, pande zote zimeeleza hoja zao na zimefikia misimamo kwa njia ya hotuba katika majukwaa, njia ambayo kwa maoni ya ACT Wazalendo inaona si njia muafaka kwa mazingira ya jambo hili na hali tuliyofikia kama Taifa
(IV) Kwamba ACT Wazalendo inatoa wito kwa pande zote mbili kutuliza vichwa na kutoa nafasi kwa hekima na busara za uongozi ili zitumike kupata ufumbuzi na suluhisho muafaka
(V) Kwamba katika hatua hizo, ACT Wazalendo inawaomba CHADEMA kuahirisha maandamano yao ya Septemba 23.2024 na pia kuiomba serikali na Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kupunguza joto na kutuliza hali ili kujenga azingira ya mazungumzo ya dhati yanayolenga kupata ufumbuzi sahihi wa mambo yote yanayolalamikiwa na pande zote
(VI) Kwamba Tanzania inayo hazina ya watu wenye busara na hekima wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wetu wa Dini ambao wakifanya kazi pamoja wanaweza kututoa kwenye hali hii iliyopo sasa na tukatoka tukiwa imara zaidi kama Taifa na hata kuwa mfano kwa wengine kama ilivyo historia etu adhimu
(VII) Mimi (Dorothy Manka Semu, Kiongozi wa ACT Wazalendo) binafsi na Mwenyekiti wa Chama Taifa ndugu Othman Masoud
Othman tunafanya mazungumzo na pande zote mbili katika jitihada za kupata muafaka wa hali tuliyonayo, tunaomba Watanzania wote tuungane katika hili
Ni sehemu ya taarifa ya a Chama cha ACT Wazalendo iliyotolewa na Kiongozi wa chama hicho Dorothy Semu iliyobeba kichwa kisemacho, ‘Wito Wetu Kwa Taifa Letu’