Latest Posts

ACT WAZALENDO YALAANI UKOSEFU WA HUDUMA BORA KWA WAZEE, YATAKA MABADILIKO YA SERA ZA PENSHENI

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, ametaka serikali ya Tanzania kutekeleza sera za afya na ustawi wa wazee, akisema kwamba licha ya mchango mkubwa wa wazee nchini, wengi wao wanaendelea kuishi katika hali ya umaskini na kukosa huduma muhimu.
 
Akizungumza Oktoba 1, 2024, wilayani Tunduru mkoani Ruvuma katika maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, Semu amesema kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa kutoa huduma bora kwa wazee.
 
“Sera na mikakati iliyopo bado haijaweza kuwasaidia wazee wetu kwa kiwango kinachostahili. Wazee wengi wanakosa pensheni, hawana bima ya afya, na wanaishi katika mazingira duni.” Amesema Semu.
 
Semu amesisitiza umuhimu wa serikali kuboresha huduma za matibabu kwa wazee na kuhakikisha wazee wote, bila kujali kama walifanya kazi rasmi au la, wanapata pensheni. Amesema kuwa serikali inapaswa kuanzisha mfumo wa pensheni kwa wazee wote ili kuwaruhusu kuishi maisha ya heshima baada ya kustaafu.
 
“Tusingekuwa na Tanzania iliyo huru kimamlaka ya kujitawala kama nyinyi Wazee wetu msingejitoa kupigania Uhuru na tunashukuru Wazee wetu kwa kubeba jukumu zito la kulea kizazi hiki, kutufundisha thamani za uadilifu, heshima na kazi.” amesema Semu.
 
Semu pia ameelezea umuhimu wa kuanzisha mpango wa bima ya afya kwa wote, akisema kuwa hii ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa wazee wanapata huduma za matibabu bila vikwazo vya kifedha. Ameongeza kuwa taifa linalosahau wazee wake ni taifa linalosahau mizizi yake, na akawataka Watanzania wote kutambua umuhimu wa kuwaheshimu na kuwatunza wazee.
 
Aidha, Semu amewakumbusha wazee kushiriki kikamilifu katika chaguzi zijazo, akieleza kuwa mwaka 2024 utakuwa wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka 2025 uchaguzi mkuu.
 
“Sasa niwaombe wazee wetu uchaguzi huu tunawakabidhi mikononi mwenu tuweze kuvuka na kushinda tuweze tekeleza sera ya ACT Wazalendo juu ya Wazee kupata Pensheni, huduma za afya bora na maisha yenye heshima”, amesema Semu.
 
Kwa kumalizia, Semu amewapongeza wazee kwa mchango wao mkubwa kwa taifa na akawahimiza vijana na serikali kwa ujumla kuwaenzi wazee kwa kuzingatia mchango wao katika kujenga taifa

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!