Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu, ameungana na viongozi wa vyama vingine vya siasa vyenye usajili wa kudumu nchini Tanzania, kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi katika makao makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma, hatua inayoashiria maandalizi rasmi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
ACT Wazalendo, moja ya vyama vinavyotajwa kufanya vizuri kisiasa pamoja na CCM na Chadema, kimeonesha tofauti ya msimamo na Chadema, ambao wametangaza kutohudhuria kikao hicho kwa sababu ya kutopatiwa majibu ya barua yao kwa Tume tangu mwaka jana pamoja na kuendelea kutokuwa na imani na Tume hiyo. Chadema wameendelea kushikilia msimamo wa vuguvugu la No Reforms, No Election.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, ameeleza kuwa maadili hayo yameandaliwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ambapo Tume, baada ya kushauriana na vyama vya siasa na Serikali, huandaa na kuchapisha kanuni hizo katika Gazeti la Serikali ili kuweka utaratibu wa mwenendo wa vyama na wadau wote wakati wa kampeni na uchaguzi.
ACT Wazalendo, licha ya kuendelea kusisitiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi, imekuwa ikifanya makongamano mbalimbali nchi nzima, yakilenga kusukuma ajenda ya uchaguzi huru na wa haki bila kususia uchaguzi huo. Tayari Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, ametangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT Wazalendo, huku makada wengine wakiwa wameonyesha nia ya kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali.