Chama cha ACT Wazalendo kimeunga mkono madai ya wananchi wa Ngorongoro kupinga kunyang’anywa haki yao ya kupiga kura, madai ya kufanyika kwa oparesheni za kuwaondoa kwenye ardhi yao na vitendo vya ukandamizaji vinavyodaiwa kufanywa na serikali dhidi yao
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa Jumatatu Agosti 19.2024 na Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho Isihaka Mchinjita imeeleza kuwa ACT Wazalendo inawapongeza wamaasai wa Ngorongoro kwa ujasiri walionesha Agosti 18.2024 kwa kuandamana kuanzia vijana, watoto, wanawake na wazee kuikabili dola na kuionesha Dunia kile walichodai kuwa ni udhalimu wanaoupitia.
Mchinjita ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara amedai kuwa serikali imekuwa ikiminya huduma za msingi (maji, afya, elimu na miundombinu ya Barabara), kuzuia shughuli za kujipatia chakula (kilimo) na malisho ya mifugo ili kutoa shinikizo la kuwaondoa wananchi wa Ngorongoro kupisha wageni na wanyama
“Sasa hivi imeenda mbali zaidi kwa kuwanyima haki ya kupiga kura kwa kuondoa majina ya baadhi ya wananchi kwenye daftari la wapiga kura, maandamano ya wananchi wa Ngorongoro dhidi ya dhamira na majaribio ya serikali kupora haki za kiraia na ardhi ni mfano wa kuigwa na unawajaza ujasiri wananchi wengine, hasa suala la ardhi ambalo kila kona ya nchi, wananchi wanalalamikia serikali kuegemea zaidi kwa wawekezaji na uhifadhi huku ikipuuza haki za wananchi” -Mchinjita
Aidha, ACT Wazalendo imewatia moyo Wamasai wa Ngorongoro kuendelea kubaki imara kupigania madai na haki zao, ujasiri na kwamba dhamira yao ni mwanga wa matumaini na wito kwa wanachi wengine nchini wanaopitia mazingira ya uonevu na ukandamizaji
ACT Wazalendo imeendelea kutoa wito kwa serikali kuruhusu haki ya ardhi kwa wananchi wa Ngorongoro kama ilivyo kwa Watanzania wengine, pia wameitaka isitishe operesheni za kuwaondoa kwenye ardhi yao, hiyo ikienda sambamba na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngoronoro (NCAA) kuvunjwa na kuundwa kampuni yenye ushiriki na umiliki wa ubia kati ya serikali na wananchi wa Ngorongoro ili kumaliza mgogoro
Chama hicho kimeapa kuendelea na dhamira ya kuunga mkono jitihada zote za kusimamia haki, kukataa udhalimu na kupinga kile walichokiita ni majaribio ya serikali na washirika wake kuporwa ardhi