Latest Posts

ACT YAITAKA SERIKALI KUWAACHIA WANANCHI KUAMUA KUHUSU ARDHI YAO

Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kuwa wakulima wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali katika utafutaji wa riziki zao ikiwamo migogoro ya ardhi na bei hafifu ya mazao yao hivyo kusababisha wakulima kuendelea kudunishwa.

Taarifa ya Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika ACT Wazalendo Mtutura Abdallah Mtutura iliyotolewa tarehe 8 Agosti, 2024, mzigo wa lawama umepewa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukikishutumu chama hicho kurahisisha “uporaji wa ardhi” na kuchochea migogoro katika ardhi, hususani baina ya kundi la wakulima na wafugaji.

“Tunashuhudia vilio vya wananchi kila kona ya nchi kuporwa ardhi na serikali na taasisi zake na vivyo hivyo na wawekezaji kupitia serikali. Hali hii inatishia maendeleo ya wakulima na kuwadidimiza katika lindi la umaskini” Ameeleza Mtutura katika taarifa hiyo.

Aidha Mtutura ameeleza kuwa bado serikali haijaweka mkazo kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ikilinganishwa na nchi zingine huku utegemezi wa pembejeo za kilimo kutoka nje ukiongezeka.

“Bado tuna huduma duni za ugani; tuna utegemezi mkubwa wa mbolea kutoka nje na hivyo tumekuwa na uhaba wa mbolea na wakati huo huo, bei ya mbolea imezidi kuwa juu na kuwa tatizo kwa wakulima. Katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia na ushindani, asilimia 86 ya wakulima bado wanatumia jembe la mkono na sekta ya viwanda haijibu changamoto za kilimo” Ameeleza Mtutura.

Kutokana na hali hiyo, ACT imeitaka serikali kuwapa mamlaka wananchi kuamua kuhusu ardhi zao kupitia mikutano ya vijiji ili kutoa ridhaa ya uwekezaji, uhifadhi au matumizi mengine.

“tunaisisitiza serikali kuanzisha fao la bei za mazao kwa wakulima na kutunga sheria ya kilimo ili kumnusuru mkulima na anguko la bei na kuhakikisha anabakia na sehemu kubwa ya mapato yake” Ameeleza Mtutura.

Aidha chama hicho kimependekeza kuwa ili kuwepo tija katika uzalishaji ni lazima serikali ifungamanishe kilimo na viwanda ili kupata nyenzo za kisasa, mbolea na uhakika wa bei za mazao na bidhaa za viwandani, kuweka msisitizo kwenye viwanda na kuongeza bajeti ya kilimo kufikia 20% ya bajeti kuu ya Serikali kutoka wastani wa asilimia 2.2 wa sasa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!