Latest Posts

ACT YAMTAKA WAZIRI WA ARDHI KUCHUNGUZA MADAI YA VIONGOZI KATA WA CCM KUPORA ARDHI YA WANANCHI

Makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Isihaka Mchinjita amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchunguza madai ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ngazi za kata na wilaya kuhusika katika uporaji wa ardhi ya wananchi na kutoa hati zisizo halali.

Mchinjita amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Lulindi, wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara alipokuwa akifanya ziara yake ya kukagua mikoa sita iliyoanza tarehe 22 Julai 2024 ambapo amesisitiza kuwa uchunguzi ufanyike na wahusika wapewe adhabu au kuvuliwa vyeo ili wananchi wapate haki yao.

 

 

“Ardhi ya nchi yetu inatosha, lakini wakulima wamekuwa wahanga wa shida hii ya kuporwa ardhi,” Amesema Mchinjita.

Aidha, Mchinjita amemwomba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuangalia upya mfumo wa ugawaji wa pembejeo kwani mfumo uliopo sasa unawaacha wakulima wengi bila pembejeo, hali inayoweza kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa korosho.

“Waziri wa Kilimo atafute mbinu mbadala ili wananchi wapate pembejeo, kwani serikali imeweka fedha za kutosha kwa ajili ya pembejeo kwa wakulima wa korosho ili uzalishaji uongezeke,” Ameongeza Mchinjita.

Naye Naibu Mwanasheria wa ACT Wazalendo, Bonifasia Mapunda amewaahidi wananchi kuwa chama hicho kimepambania sheria mpya ya uchaguzi ya mwaka 2024, pamoja na sheria ya tume huru ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.

Amesema sheria hizo zinalenga kuleta mabadiliko, na ACT Wazalendo itahakikisha zinatekelezwa.

Kwa upande wake Katibu wa Ngome ya Wazee wa ACT Janet Fussi, amewataka wananchi kujiunga na ACT Wazalendo ili kujikomboa kutoka kwenye utawala wa CCM ambao amedai umeshindwa kuona mahitaji ya wanawake wajawazito, wanaokabiliwa na changamoto za kutafuta huduma za afya katika zahanati za vijiji na upungufu wa magari ya wagonjwa (ambulance).

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!