Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakiwezi kunyamaza kimya endapo CHADEMA itakandamizwa, kikisisitiza mshikamano wake na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Akizungumza katika kikao cha ndani cha chama hicho kilichofanyika wilayani Kilwa, mkoani Lindi, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amesema chama chake hakiwezi kufumbia macho matukio yanayoikumba CHADEMA, ikiwemo kuzuiwa kwa mikutano yao na kutoweka kwa baadhi ya viongozi wao.
“Baadhi ya watu wametuhoji kwa nini ACT inakuwa sauti ya CHADEMA. Leo nataka niwaambie Wanakilwa, ikiumizwa CHADEMA tukakaa kimya, anayefuata ni nani? Ni sisi ACT Wazalendo. Ikiumizwa CHADEMA tuchukulie kwamba tumeumizwa na sisi,” amesema Shaibu.
Akiendelea kusisitiza mshikamano huo, amesema ACT Wazalendo inachukizwa na jeshi la polisi kwa kile alichokiita upendeleo wa wazi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa mikutano ya chama tawala hupewa ulinzi mkubwa kwa kusindikizwa na gari za polisi, huku mikutano ya upinzani ikizuiwa.
“Tunafahamu viongozi wao wawili hawaonekani mpaka sasa katika kipindi cha wiki chache zilizopita. Tunafahamu pia kuwa jeshi la polisi limezuia mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliopangwa kufanyika Machi 25, 2025, kule Mbarali, Mbeya. Ninawaambia ndugu zetu wa CHADEMA tupo pamoja, tutashirikiana, na tunalionya jeshi la polisi kwa kufanya kazi kwa ubaguzi. Kwa nini CCM wanapewa mpaka magari ya polisi yanasomba watu kwenye mikutano yao, lakini mikutano ya upinzani inawekewa vikwazo?” amehoji.