Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kutoshiriki vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa vinavyotarajiwa kufanyika tarehe 12 na 13 Machi, 2025, kikieleza kuwa baraza hilo limepoteza uhalali wake wa kuwa jukwaa la majadiliano ya kisiasa nchini.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa tarehe 11 Machi, 2025, na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, ACT Wazalendo imesema kuwa Baraza la Vyama vya Siasa limeshindwa kutimiza lengo lake kuu la kukuza misingi ya demokrasia ya vyama vingi nchini.
ACT Wazalendo inadai kuwa baraza hilo limegeuzwa kuwa chombo cha kuhalalisha na kusafisha ukiukwaji wa demokrasia, hususan katika chaguzi mbalimbali za nyuma, ikiwemo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Pia chama hicho kimelaumu serikali kwa kupuuza maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa cha tarehe 11 Oktoba, 2024, ambacho kilikuwa na lengo la kuboresha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024.
“Serikali, kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilitoa ahadi ya kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa. Kinyume cha ahadi yake ambayo ilitolewa kimaandishi, Serikali iliyatupa mapendekezo ya Baraza la Vyama vya Siasa na kuendelea na mpango wake wa kudhulumu sauti ya wananchi kupitia wizi wa kura na uchafuzi kama ilivyoshuhudiwa nchi nzima”, ameeleza Ado.
Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo imetoa wito kwa serikali kuweka bayana kalenda ya utekelezaji wa mabadiliko muhimu ya mfumo wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, kuharakisha marekebisho ya sheria za uchaguzi, ikiwemo Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na mabadiliko ya Katiba yatakayohakikisha uchaguzi huru na wa haki.
“ACT imewasilisha tena kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye Katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa uchambuzi wake wa kina wa masuala yanayohitaji kufanyiwa maboresho katika tasnia ya siasa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu 2025 unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika”, ameeleza Ado