Latest Posts

ACT YATOA WITO KUHUSU UBAGUZI WA WAGOMBEA KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza wasiwasi wake kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa nafasi za uongozi katika Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji, baada ya kupokea taarifa zinazoonesha kuwa wagombea wake wamekataliwa kwa sababu ambazo zinaonekana kukiuka misingi ya haki na uwazi wa uchaguzi.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa tarehe 8 Novemba 2024, Rahma Mwita, Msemaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa chama hicho, amesema kuwa ACT Wazalendo imepokea malalamiko kutoka kwa wagombea wake ambao wametengwa kinyume na kanuni za uchaguzi.

Mwita amefafanua kuwa baadhi ya sababu zilizotumika kuwazuia wagombea hao ni pamoja na kutokamilisha fomu za uteuzi; bila kuelezwa kwa kina juu ya kasoro hizo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, udaiwa kutokuwa wakazi wa maeneo wanayotaka kugombea; madai ambayo chama kinasema hayana ushahidi wa kutosha, na kukosa kazi; wagombea kuenguliwa kwa msingi wa kutokuwepo na uthibitisho wa ajira, hatua ambayo ACT Wazalendo imepinga kwa kusema ni ukiukwaji wa haki zao kikatiba.

ACT Wazalendo imetoa wito kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, kuhakikisha kuwa wagombea wote waliotengwa wanarejeshwa kwenye orodha ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

“Ni muhimu kwa TAMISEMI kuhakikisha kuwa mchakato huu unazingatia misingi ya haki na kanuni za uchaguzi ili kila mgombea mwenye sifa apate nafasi ya kugombea,” amesisitiza Mwita.

Aidha, chama hicho kimewataka wagombea wake wote walioathirika na uamuzi huo kukata rufaa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, huku wakiendelea na juhudi za kuhakikisha haki zao zinatimizwa. “Tumetoa maelekezo kwa wagombea wetu kukata rufaa dhidi ya maamuzi haya ili kudai haki yao,” ameongeza Mwita.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa ACT Wazalendo itaendelea kupambana kwa ajili ya haki na usawa wa kidemokrasia nchini Tanzania, hasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!