Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha kwa kushirikiana na Chuo Cha Uongozi wa Elimu ADEM wanatarajia kuanzisha mpango wa pamoja wa kutoa mafunzo kwa walimu nchi nzima, ili kuboresha sekta ya elimu na kujenga uzalendo miongoni mwa walimu na wanafunzi. Mpango huo ulitangazwa na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha ADEM, Dkt. Maulid Maulid, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo walimu wakuu wa Wilaya ya Ilala yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha.
Dkt. Maulid amesema wamekubaliana na uongozi wa shule hiyo kuanzisha utaratibu wa mafunzo ya wiki moja kwa walimu wakuu wote nchini, kwa lengo la kuwaimarisha kitaaluma na kiuongozi. Alieleza kuwa ADEM inatoa elimu ya uongozi kwa walimu huku Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere ikitoa elimu ya uongozi kwa ujumla, ikiungwa mkono na miundombinu bora ya malazi kwa walimu.
Kuhusu ukatili dhidi ya watoto, Dkt. Maulid alisisitiza kuwa kila mmoja anawajibika kuhakikisha usalama wa mtoto kuanzia ngazi ya familia, jamii, na mamlaka nyingine za elimu. Alisema changamoto ya afya ya akili kwa baadhi ya walimu imekuwa chanzo cha kutoa adhabu kali kwa wanafunzi, hivyo wameamua kuanzisha mpango wa mafunzo ya mara kwa mara kwa walimu wakuu ili kuimarisha miiko ya uongozi shuleni.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, John Baitan, alisema mafunzo hayo yamewapa walimu maarifa katika nyanja za usalama wa nchi, itifaki, uzalendo, umajumui, usimamizi wa fedha za serikali, pamoja na mbinu za kuongeza mapato kwa kufuata sheria. Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uwezo wa kiutendaji wa wakuu wa shule za sekondari.
Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Sekondari Jiji la Dar es Salaam (Dar City), Mwalimu Boniface Mwalwego, alisema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uwajibikaji, kuimarisha nidhamu mashuleni, na kusaidia utekelezaji wa sera na mitaala ya elimu. Aliongeza kuwa asilimia 75 ya washiriki wa mafunzo hayo ni wakuu wa shule wapya ambao walikuwa hawajapatiwa mafunzo rasmi tangu mwaka 2020, hivyo hatua hii imekuja wakati muafaka wa kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi.