Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Stephen Wasira, ni mbinu ya kimkakati ya chama hicho ili kuzuia mijadala kuhusu Katiba Mpya.
Akizungumza Februari 10, 2025 wilayani Mkuranga mkoani Pwani, alipokuwa akihitimisha ziara yake katika mkoa wa kichama wa ACT wa Mwambao (wenye majimbo ya Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Mafia), Ado amedai kuwa CCM inataka upinzani usahau madai ya Katiba Mpya na badala yake ujikite kwenye mijadala kuhusu Wasira.
“Sasa hivi ameletwa mbabaishaji anayeitwa Stephen Wasira. Hii ni mbinu ya CCM ya kuhamisha ajenda. Wanataka tuache kudai Katiba Mpya na badala yake tujadili hoja zake za kitoto,” amesema Ado.
Amesema kauli ya Wasira kwamba “Watanzania hawali Katiba Mpya” ni dhihaka kwa wananchi, kwani maendeleo kama maji na barabara hayawezi kupatikana bila mfumo mzuri wa uongozi.
“Mzee Wasira anataka kupoteza muda wetu, badala ya kudai Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya, tunahangaika naye. Dawa yake ni kumuacha na kuendelea kupigania haki ya Watanzania,” amesema Ado.