Nchi ya Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano unaowakutanisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Wataalamu wa Tiba kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya kwa Nchi za Afrika (ISSUP- AFRICA).
Akizungumzia mkutano huu unaofanyika kwa siku mbili mkoani Arusha kuanzia tarehe 21 mpaka 22 Agosti, 2024, Mkurugenzi Mkazi wa ISSUP Tanzania Dkt. Cassian Nyandindi amesema kuwa mkutano huo unalenga kuangazia namna bora ya kuimarisha utoaji wa elimu sahihi kwa umma kuhusiana na masuala ya dawa za kulevya na kuimarisha tiba na huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa hizo.
Amesema katika mkutano huo watajadili mada mbalimbali ikiwamo ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya duniani na Afrika, na namna ambavyo mataifa ya Afrika yanaweza kutumia njia sahihi zilizothibitishwa kisayansi ili kuwanusuru watu walioathirika na dawa za kulevya.

“Tutaangalia na kupanga namna bora ya kufanya utafiti wa pamoja kwa maana ya kuboresha huduma lakini pia kujua ukubwa wa tatizo ili tuweze kujipanga zaidi katika utekelezaji wa majukumu yetu na kutengeneza sera thabiti ambazo zitatumika kupambana na tatizo hilo”, ameeleza Nyandindi.
Aidha amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo unakuja na fursa tofauti kwa Watanzania ikiwamo ubadilishanaji uzoefu baina ya wataalamu wa Tanzania na nje ya nchi, na fursa za utalii.
“Hii ni fursa kwa nchi yetu kutangaza utalii nchini ndiyo maana tumechagua mkutano huu ufanyike Arusha na baadhi ya wageni watakaotoka hapa watakuwa ni mabalozi wazuri wa kuitangaza nchi yetu na wengine wataendelea kubaki hapa kwa ajili ya kufanya utalii”, ameeleza Nyandindi.

Mkutano ISSUP unafanyika kila mwaka ambapo mwaka 2024 Tanzania imeteuliwa kuwa nchi mwenyeji na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ndiyo taasisi mwenyeji kwa Tanzania.
Mkutano huu unajumuisha nchi 16 za Afrika, wataalamu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linashoghulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Umoja wa Nchi za Afrika (AU) pamoja na wawakilishi kutoka makao makuu ya ISSUP.
