Usiku wa giza la Septemba 6, 2024, barabara ya Morogoro – Dar es Salaam iligeuka kuwa eneo la huzuni na mshtuko, baada ya magari matatu kugongana eneo la Mikese, na kusababisha vifo vya watu wanne na kujeruhi wengine 15.
Kati ya magari hayo, lilikuwepo basi la kampuni ya Kibisa, lori lililokuwa limebeba vinywaji, na gari dogo aina ya Wish.
Scholastica Ndunga, Kaimu Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, alizungumza na tovuti ya Mwananchi kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo kuhusu tukio hilo, na kuthibitisha kuwa miili ya marehemu wanne ilihifadhiwa hospitalini hapo, huku majeruhi 15 wakipatiwa matibabu.
“Awali tulipokea miili ya watu watatu waliofariki papo hapo, lakini majeruhi mmoja alifariki baadaye asubuhi hii, hivyo kufanya idadi ya vifo kufikia wanne.”alieleza Ndunga
Mmoja wa manusura wa ajali hiyo, Ally Kipande, aliyekuwa akisafiri na basi la Kibisa kuelekea Dar es Salaam, alisimulia jinsi lori lilivyoyumba na kupoteza mwelekeo, likaligonga basi lao uso kwa uso kabla ya kuligonga gari dogo.
“Nilishuhudia wenzangu wakitoka wakiwa wamekufa,” alisema Kipande kwa huzuni, huku akitoa shukrani kwa Mungu kwa kunusurika kwenye ajali hiyo.
Aidha amesema kwa namna alivyoona ajali hiyo ilivyotokea, anaweza kusema chanzo ni dereva wa lori lililobeba vinywaji ambaye alitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na hivyo alianza kuyumba na kupoteza uelekeo, kisha kuligonga basi hilo.
Kwa mujibu wa Mwananchi, kamanda wa polisi wa Morogoro, Alex Mkama bado hakuweza kupatikana kutoa maelezo zaidi juu ya chanzo rasmi cha ajali hiyo.