Chama cha ACT Wazalendo kimetoa msimamo wa kuunga mkono na kuongoza mapambano ya wananchi katika kukabiliana na wimbi kubwa la kile ilichokiita kuwa ni uporaji wa ardhi nchini, viongozi wa chama hicho wameeleza masikitiko yao baada ya kukutana na kero nyingi za migogoro ya ardhi, uporaji na oparesheni za serikali zinazolenga kuwaondoa wananchi kwenye ardhi yao karibu kwenye kila jimbo walilopita kwenye ziara inayoendelea kufanywa kila koja hapa nchini vitendo vinayodaiwa kuondoa usalama na uhakika wa milki ya ardhi kwa wananchi na kudhoofisha maendeleo yao, hivyo kutoa wito wa kukomesha
Msimamo huo umetolewa na viongozi wakuu wa ACT Wazalendo wanaoendelea na ziara ya awamu ya kwanza ya kuyafikia majimbo 214 ya Tanzania Bara wakiwa kwenye majimbo ya Bunda Vijijini (Mara), Mbulu (Manyara), Newala mjini (Mtwara) na Kigoma Kusini (Kigoma)
Akiwa Mbulu mkoani Manyara Kiongozi wa Chama Dorothy Semu amesema ACT Wazalendo inapata wasiwasi kukikithiri kwa malalamiko ya wananchi kwenye ardhi na kwamba hatua zinazochukuliwa na serikali hazisaidii kulinda haki za wananchi hao.
“Migogoro ya ardhi nchini kwetu inazidi kuongezeka, wafugaji na wakulima, wananchi dhidi ya serikali, wananchi dhidi ya wawekezaji kwa nyakati zote waathirika ni wananchi, wao ndio wanapoteza haki zao za kutumia ardhi, mara kadhaa tunashuhudia mauaji, mapigano, kufukuzwa au uhamishaji wa wananchi kwenye ardhi zao” -Semu
Ameeleza kuwa, kiini cha matatizo yote wanayopitia wananchi kwenye ardhi ni ardhi kuwekwa kwenye mikono ya Rais, hivyo serikali kujipa mamlaka ya mwisho katika kutwaa, kudhibiti na kumiliki ardhi bila ridhaa ya wananchi
“Nataka niwaambie mfumo huu unamfanya Rais kuichezea ardhi kwa utashi wake, akipata mteja wa kufuga wanyama sehemu yoyote ya ardhi nchini anaweza kuwaondoa watu kwenye ardhi hiyo ili tu kumpisha huyo mtu afuge, hii ndio maana ya yote tunayoyaona” -Semu
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara Isihaka Mchinjita amesema kasi ya kupandisha hadhi na kupanuliwa kwa maeneo ya hifadhi imeongeza migogoro, kwa kuwa ananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo wameishia kuporwa ardhi, kupitia ukandamizaji, udhalilishaji na mateso makubwa.
“Serikali imekuwa ikipanua maeneo ya hifadhi kwa kumega ardhi za wananchi kwa kutumia nguvu kubwa, wakati tunapata uhuru eneo lote la hifadhi lilikuwa sawa na 12% ya ardhi yote huku tukiwa na idadi ndogo ya watu, kwa sasa eneo la hifadhi linachukua 38% ya ardhi yote na sasa tunasikia tetesi kwamba serikali inataka kuongeza eneo la hifadhi kufikia 50% ya ardhi” -Mchinjita
Amesisitiza kuwa serikali ya CCM inajali zaidi wanyama na wawekezaji kwa kuwa inachukulia ardhi inapaswa kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji ya kijamii, ndio maana inapora ardhi kutoka kwa wananchi wazawa na kuanzisha ‘hifadhi’ kwa ajili ya wawekezaji
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu ameeleza mfumo na sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kuwa na mapungufu yanayotishia haki na usalama wa ardhi za wananchi vijijini, amesema mfumo uliopo wa mabaraza hauna utaratibu wa uwajibikaji kwa kuwa unasimamiwa na mamlaka zaidi ya moja, ametaja mapungufu mingine ya kiuendeshaji kama vile uelewa mdogo wa wajumbe katika mabaraza ya vijiji na kata, rushwa na upendeleo.
“Nchi yetu kuna ardhi ya kijiji na ardhi ya jumla, wananchi vijijini wanapoteza ardhi kutokana na viongozi wabovu wa vijiji, wengi wao ni wala rushwa, wababe na hawawashirikishi wananchi, wanapora mamlaka ya mkutano wa kijiji kwenye kuamua masuala ya ardhi kama sheria inavyotaka” -Ado
Naye, Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe akiwa Ilagala Kigoma Kusini (Kigoma) amedai kuwa anaona kila dalili ya kutokea vita nchini itakayohusisha ardhi, akidai kuwa vita hiyo itakuwa kati ya kundi la wakulima na wafugaji.
Akieleza sababu kubwa ya hofu yake amesema malalamiko juu ya migogoro ya ardhi yamekuwa makubwa na yanazidi kuongezeka badala ya kupungua.