Na Amani Hamisi Mjege.
Mwaka 2024 unashuhudia kuzinduliwa kwa Jukwaa la Ajenda ya Msichana 2024, mradi wa kipekee unaolenga kuwainua wasichana katika uongozi kwa kutumia teknolojia ya kidijiti.
Uzinduzi huo unafanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike (IDGC), ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 11 Oktoba.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano Septemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam, Esther Japhet Abduely ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Boma, akifanya kazi na shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wasichana na Uongozi Kupitia Teknolojia ya Kidigitali.”
Ameongeza kuwa wadau saba wa haki za wasichana nchini Tanzania, wakiwemo Msichana Initiative, GLAMI, TAI, na Young Strong Mothers Foundation, wameungana katika kuendesha kampeni hii ili kutoa mafunzo na hamasa kwa wasichana katika mikoa mbalimbali, lengo kuu ni kuhakikisha kuwa wasichana wanapata fursa sawa za uongozi, na pia kutumia teknolojia kuboresha nafasi zao katika jamii.

Matukio mbalimbali yamepangwa kufanyika kuanzia tarehe 12 Septemba 2024, katika mikoa ya Arusha, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Dodoma, Mbeya, na Zanzibar, yakishirikisha wasichana wapatao 5,000, na wasichana 200 watakutana Dodoma kwa maadhimisho ya kilele wakiwawakilisha wengine.
Angel Mohamed, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Einoti kutoka Arusha akifanya kazi na taasisi ya GLAMI, ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wasichana bado hawajawahi kushiriki katika mchakato wa uongozi, hali inayochangiwa na vikwazo vya kijamii na kifamilia.
“Tafiti zinaonesha kuwa 44.4% ya wanafunzi wa Sekondari hawaelewi maana ya demokrasia, huku 85.5% hawajawahi kushiriki, kushirikishwa katika vikao rasmi vya shule vinavyofanya uamuzi. Pia, 68.9% ya wanafunzi hawajawahi kugombea au kuonesha nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ngazi ya shule, huku 44% hawashiriki katika chaguzi za uongozi wa wanafunzi”, ameeleza Angel.

Naye Sharifa Jumanne Ally, mwanafunzi kutoka chuo cha biashara cha CBE, na akifanya kazi na taasisi ya C-Sema amesema mada muhimu zitajadiliwa katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na changamoto na fursa zinazowakabili wasichana katika sekta za elimu, afya, na kijinsia, huku washiriki wakisikia ushuhuda wa wasichana waliofanikiwa kupitia nafasi za uongozi.
Brian Terry, Mratibu wa Jukwaa la Ajenda ya Msichana kutoka Flaviana Matata Foundation, ametoa shukrani kwa washiriki wote kwa kujitolea kuhakikisha uzinduzi huo unafanikiwa. Amesisitiza kuwa safari hii ni ya pamoja na kila mmoja ana jukumu la kujenga mazingira bora kwa mtoto wa kike.
“Ni muhimu tukumbuke kuwa safari hii ni ya pamoja. Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha kuwa tunajenga mazingira ambayo yatampa mtoto wa kike nafasi ya kustawi, kujifunza, na kutumia vipaji vyake kikamilifu,” alisema Terry.