Katika hali isiyokuwa ya kawaida aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu Yahaya Ismail Nawanda ameibua mjadala mkubwa baada ya kuibuka kwa tahuma dhidi yake akidaiwa kumlawiti binti mmoja mwenye umri wa miaka 21 mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya ugavi na manunuzi anayesoma katika Chuo Kikuu cha St. Augustine, jijini Mwanza.
Barua ya ‘siri’ ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza iliyoandikwa Juni 04.2024 ambayo imesainiwa na ASP Felician Lyope kwa niaba ya Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani humo iliyotumwa kwa Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai, makao makuu ya Polisi (upelelezi) Dodoma imedai kuwa mnamo Juni 03.2024 majira ya Saa 05:00 asubuhi katika jengo la Ofisi ya Mkuu wa mkoa Mwanza alifika binti huyo na kuomba kukutana na wahusika wanaoshughulikia masuala ya haki za binadamu, maafisa waliompokea na kumsikiliza walimshauri binti huyo kupeleka taarifa hizo kituo cha Polisi (Dawati la Jinsia na Watoto), ndipo binti huyo alipofika kwenye dawati hilo ambapo alikutana na kiongozi wa dawati hilo mkoa wa Mwanza aliyetajwa kwa jina la Inspekta Faraja.
Inaelezwa kuwa katika maelezo yake mbele ya Afisa huyo wa Jeshi la Polisi, binti huyo alieleza kuwa Juni 02.2024 majira ya saa 02:00 usiku katika maegesho ya magari ya bar maarufu jijini Mwanza iitwayo ‘The Cask’ alilawitiwa na mwanaume mmoja aitwaye Nawanda ambaye kwa majina mengine anafahamika kama Yahaya Ismail, ambapo amedai kuwa mwanaume huyo alimfanyia kitendo hicho baada ya kumpigia simu na mtuhumiwa ambapo alimuomba kufika kwenye bar hiyo kwa ajili ya mazungumzo lakini alipofika kwenye eneo hilo alielekezwa kuingia kwenye gari moja aina ya Toyota Crown nyeupe ambaye hakuweza kutambua namba zake za usajili, na alipoingia kwenye gari hiyo alimkuta mtuhumiwa akiwa ameketi kwenye kiti cha dereva ndipo mazungumzo yao yalipoanzia.
Barua hiyo ya ‘siri’ ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza imefafanua kuwa katika mazungumzo yao mlalamikaji anadai kuwa mwanaume huyo alikuwa anamsihi akubali kufanyanae mapenzi kinyume na maumbile lakini mlalamikaji alidai kuwa hajawahi kufanya kitendo cha aina hiyo, hata hivyo inatajwa kuwa mtuhumiwa alizidi kumbembeleza mlalamikaji akimsihi kuwa asiogope kwa kuwa kwa mara ya kwanza atasikia maumivu lakini baadaye atazoea, na katika hilo inadaiwa kuwa mtuhumiwa aliahidi kumbadilishia mlalamikaji hali ya maisha yake kiuchumi kwa kumpatia Tsh. 500,000/- (laki tano) kila mwezi sambamba na kumsaidia dada yake (jina linahifadhiwa) kupata ajira.
Inaelezwa kuwa wakati mjadala wao ukiendelea ndipo mwanaume huyo alimfunua sketi, chupi na blauzi kisha kumlawiti huku akimtishia kuwa asihangaike kupiga kelele kwa sababu gari lake linafahamika na kuna walinzi wamelizunguka hivyo hawezi kupata msaada wowote, baada ya ukatili huo kutendeka ndipo mwanaume huyo alifungua mlango wa gari na mlalamikaji kuondoka kupitia geti la Ghana, na mtuhumiwa aliondoka kwa miguu kuelekea kwenye bar nyingine iitwayo ‘Sato Sangara’.
Inaelezwa kuwa baada ya kutendewa tukio hilo mlalamikaji alielekea Malimbe katika Hosteli ya wanafunzi wa Chuo cha St. Augustine (SAUT) iitwayo South Village ambapo anaishi peke yake katika chumba namba 15 ambapo alivua nguo alizovaa siku hiyo na kuziweka kwenye kapu la nguo chafu kisha kulala huku akisikia maumivu makali mwilini, ndipo alipofikia maamuzi ya kumpa taarifa mama yake mzazi anayeishi Mpanda mkoani Katavi, mama yake mzazi alimshauri binti yake kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vya kisheria ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa, ndipo mlalamikaji alipotoa taarifa hizo katika dawati la jinsia na watoto ambapo alitoa maelezo yake kwa maandishi, baadaye Inspekta Faraja alimfikisha mtendwa Hospitali ya Sekou Toure kwa uchunguzi wa kitaalamu.
Barua hiyo ya ‘siri’ kutoka Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza imefafanua kuwa mnamo Januari 20.2024 majira ya saa 02:30 usiku maeneo ya ‘The Cask Bar’ wilaya ya Ilelema jijini Mwanza mlalamikaji alikutana na mtuhumiwa huyo kwa mara ya kwanza wakiwa kwenye birthday party ya mtu mmoja (jina limehifadhiwa) ambapo mtuhumiwa alikuwa pia mgeni mwalikwa, katika sherehe hiyo wawili hao walitambulishwa na kubadilishana namba za simu kwa ajili ya mawasiliano ya kirafiki, ambapo mlalamikaji na mtuhumiwa waliendelea kuwasiliana kwa njia ya simu (What’sup, video call, jumbe fupi nk) huku mtuhumiwa akimtumia mlalamikaji fedha za kujikimu.
Inaelezwa kwenye barua hiyo kuwa mnamo Februari 2024 mlalamikaji anakumbuka kuwa siku moja ambayo ilikuwa ni siku ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Dkt. Samia Suluhu Hassan) ambapo mtuhumiwa alikuja Mwanza na kumpigia simu mlalamikaji, ambapo wawili hao walikutana katika Hoteli hiyo ambapo mtuhumiwa alimueleza mlalamikaji kuwa anamtaka afanayenae mapenzi kinyume na maumbile lakini mlalamikaji alikataa katakata kuwa na mahusiano ya aina hiyo na kwa hasira aliondoka chumbani hapo bila maelewano, hata hivyo mtuhumiwa aliendelea kumbembeleza mlalamikaji ili siku moja amkubalie ombi lake la kufanyanae mapenzi kinyume na maumbile.
Habari zinasema mtuhumiwa aliendelea kumbembeleza mmlalamikaji ili siku moja amkubalie ombi lake la mapenzi kinyume na maumbile, ilipofika Juni, 02, 2024, ndipo mtuhumiwa alizidi kumbembeleza mmalamikaji wakutane ili waongee zaidi kuhusu jambo hilo.
Mlalamikaji aliamua kwenda bar ya ‘The Cask’ akidhani mtuhumiwa alibadili nia yake, pengine anataka kuomba msamaha kwa kitendo cha kumuomba mapenzi kinyume na maumbile, alipoingia kwenye gari ndipo alifanya tukio la ulawiti.
Taarifa zinasema dawati la jinsia na watoto mkoani Mwanza lilianza uchunguzi wa tukio hilo na kumuhoji mlalamikaji na kumpeleka Hospitali ya Seko Toure kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalam baada ya kupata PF3.
Imebainika kuwa katika taarifa ya kitaalam iliyotolewa na Daktari wa Hospitali hiyo (jina linahifadhiwa) ameeleza kuwa katika uchunguzi wake amebaini kuwa mlalamikaji ameingiliwa kinyume na maumbile kwa kuingiziwa kitu butu katika sehemu yake ya haja kubwa na hivyo kusababisha michubuano na maumivu.
Wataalam wa uchunguzi wa kisayansi Juni, 03, 2024 walifika katika chumba anachoishi mlalamikaji na kufanikiwa kupata nguo ambazo mlalamikaji alizivaa siku ya tukio na vielelezo vingine ambavyo vinapelekwa kwa Mkemia wa serikali kanda ya Ziwa kwa uchunguzi zaidi.
Pia, mlalamikaji amechukuliwa sampuli ya mate yake kwa ajili ya uchunguzi wa DNA huku wakisubiri mtuhumiwa atakapokamatwa aweze pia kuchukuliwa vipimo hivyo kwa hatua zaidi za upelelezi.
“Ufuatiliaji umefanyika katika eneo la tukio kwa kuangalia picha za video za CCTV Camera iliyofungwa kwenye jengo la Rocky City ambapo imemuonesha mlalamikaji akiingia kwenye gari iliyoegeshwa kwenye maegesho hayo na ilipofika saa 02:48 usiku anaonekana mmlalamikaji akiingia kwenye hilo gari baadae saa 03:12 usiku mlalamikaji anaonekana akitoka kwenye hilo gari.
“Kisha majira ya saa 06:24 usiku gari hilo linaonekana kwenye geti kwenye mwanga mkali linasomeka T 496 BND Toyota Crown nyeupe huku dereva aliyevalia kapero akitoka kwenye gari hilo kwa ajili ya kulipia ushuru wa maegesho.
Mlalamikaji ambaye pia ameshiriki katika kuangalia CCTV Camera hiyo pamoja na askari wa upelelezi alimtambua mtuhumiwa na gari na kuwaonesha askari wa upelelezi kuwa ndiye aliyemfanyia tukio la ulawiti na kuitambua hiyo gari ndogo kuwa ndiyo iliyotumika katika eneo la tukio.
“Simu ya mmalamikaji na CCTV Camera footage vinaandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye maabara ya uchunguzi wa kisayansi kwa uchunguzi zaidi, kuhusu gari T 496 BND Toyota Crown imetumwa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mwanza ili kujua uhalali wa gari.
Mtuhumiwa wa tukio hilo bado hajakamatwa na upelelezi bado unaendelea, lakini tuhumiwa amefunguliwa jalada la uchunguzi MZR/CID/PE/74/2024.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa leo, Jumanne imeeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Yahaya Ismail Nawanda aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu na nafasi yake imechukuliwa na Kenan Kihongosi aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Momba mkoani Songwe, ingawa taarifa hiyo ya Ikulu iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Sharifa Nyanga haijataja sababu ya utenguzi huo.