Kampuni ya Amsons Group ya Tanzania imejipanga kuwa kinara wa uzalishaji na usambazaji wa saruji katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa na mpango wa kujenga viwanda vipya vitatu vya saruji- viwili Tanzania na kimoja nchini Kenya na kuongeza uwezo wake wa uzalishaji kwa zaidi ya tani milioni tano katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Kampuni hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Edha Nahdi tayari imekamilisha ununuzi mkubwa wa kampuni ya Bamburi Cement nchini Kenya kwa thamani ya Shilingi za Kitanzania bilioni 500, hatua ambayo imekuwa ya kihistoria katika upanuzi wa biashara ya ndani na nje ya mipaka.
Katika mahojiano maalum ya hivi karibuni kupitia kipindi cha Connecting Africa cha CNN kilichoongozwa na mtangazaji Eleni Giokos, Edha Nahdi amefunguka kuhusu mkakati wa kampuni hiyo unaolenga kutawala soko la saruji katika ukanda huu. Nahdi ameeleza kuwa ununuzi wa Bamburi Cement ulikuja baada ya ununuzi wa awali wa Mbeya Cement kutoka kwa kampuni ya Lafarge Holcim, hatua iliyowaweka kwenye nafasi bora ya kujiimarisha kama kiongozi wa sekta hiyo.
“Kabla ya kuinunua Bamburi Cement ya Kenya, tulinunua pia kiwanda cha Mbeya Cement kutoka Lafarge Holcim, ambao pia walikuwa wamiliki wa Bamburi. Ilipokuja fursa ya Bamburi kuuzwa, tuliona inalingana kikamilifu na dira yetu ya kuwa kinara wa saruji katika ukanda huu,” ameeleza Nahdi.
Alipoulizwa kuhusu sababu ya kampuni za kimataifa kuachia vitega uchumi Afrika, Nahdi ameeleza kuwa mabadiliko ya mazingira ya kodi barani Ulaya, hususan kodi ya kaboni, yamekuwa mzigo kwa kampuni za Ulaya zenye vitega uchumi nje ya bara hilo, na hivyo kuyaacha masoko kama ya Afrika.
“Kampuni nyingi za Ulaya zinalazimika kulipa kodi ya kaboni hata kwa uzalishaji wao wa saruji Afrika. Kwa hiyo, kwao inaonekana kama mzigo. Lakini kwetu sisi barani Afrika, bado hatujafika huko. Hivyo hii ni fursa ya kipekee,” amesema.
Kuhusu utekelezaji wa Makubaliano ya Biashara Huria Afrika (AfCFTA), Nahdi amesema bado kuna changamoto hasa katika baadhi ya sekta kutokana na vizuizi vya forodha na ushuru wa kuingiza bidhaa katika baadhi ya nchi jirani.
“Katika mafuta tumefanikisha biashara kati ya nchi sita hadi saba za jirani, lakini katika sekta zingine bado kuna ushuru na ada za kuingiza bidhaa. Ndio maana kusema tupo mbali kidogo kufikia muunganiko kamili wa kibiashara Afrika,” ameeleza Nahdi.
Kuhusu mustakabali wa kampuni hiyo, Nahdi amesema kuwa Amsons Group inalenga kufikia thamani ya mauzo ya zaidi ya dola bilioni 3 katika kipindi cha miaka mitano ijayo, huku pia wakipanua uwekezaji wao katika nishati mbadala kama umeme wa jua.