Latest Posts

ANDREA LEMNGE AAGA CHADEMA: “NI HERI KUPIGANA KWA HAKI KULIKO KUISHI KWA UTULIVU WA UNYONGE”

Aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CHADEMA na Mtia nia wa Ubunge katika Jimbo la Rombo, Andrea Lemnge Oisso, ametangaza kujivua uanachama wa chama hicho akilaani msimamo wa kususia uchaguzi kwa hoja kwamba “historia haijawahi kumbeba anayekimbia mapambano”.

Akizungumza kupitia tamko rasmi lililotolewa leo, Lemnge amesema licha ya kuunga mkono misingi ya msingi ya chama hicho kwa miaka mingi, ikiwemo kauli ya “No Reform, No Election”, ameona kwamba njia ya kususa uchaguzi siyo suluhisho bali ni kujiondoa kwenye mapambano ya kweli ya kisiasa.

“Historia inaonesha wazi: hakuna chama cha upinzani kilichowahi kufanikisha mabadiliko ya msingi kwa kujiondoa kwenye uchaguzi. Kususa ni sawa na kujiuzulu kutoka kwenye mapambano- jambo ambalo dhamira yangu inashindwa kukubaliana nalo”, ameeleza.

Andrea Lemnge amesisitiza kwamba yeye ni miongoni mwa waliokuwa wakiamini kuwa mabadiliko ya kweli yanahitaji ujasiri wa kupambana ndani ya mfumo mgumu na siyo kuukwepa.

Mimi si muumini wa msimamo huo. Kuwaachia CCM kila kitu ni kuwavunja moyo Watanzania waliotazama CHADEMA na upinzani kwa matumaini makubwa. Tusiposhiriki, tutakuwa tumewasaliti. Mimi naamini: ni heri kupigana na kuumizwa kwa haki kuliko kuishi kwa utulivu wa unyonge,” amesema kwa msisitizo.

Katika hatua hiyo, amesema ataendelea kusimamia nia yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Rombo, huku akisisitiza kwamba atafanya hivyo kupitia jukwaa jingine jipya la kisiasa atakalolitangaza baadaye.

Aidha, Lemnge ameushukuru uongozi wa CHADEMA na wapambanaji wote waliompa ushirikiano kwa kipindi chote, akisisitiza kuwa anaondoka kwa heshima bila chuki wala kinyongo.

Andrea Lemnge anajiunga na orodha ya viongozi na wanachama mbalimbali wa CHADEMA waliopinga wazi msimamo wa chama wa kuzuia uchaguzi mkuu na kuhamia vyama vingine. Kwa sasa, bado hajatangaza chama kipya atakachojiunga nacho, lakini ametahadharisha kuwa “mapambano hayaishi”.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!