Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, amesema kuwa atatekeleza majukumu yake kwa haki, uadilifu na uzalendo mkubwa katika mchakato wa kujadili majina ya wagombea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza na wanachama wa CCM mkoani Iringa waliojitokeza kumpongeza kufuatia kuteuliwa kwake hivi karibuni kushika nafasi hiyo nyeti, Asas alisema kuwa nafasi hiyo ni dhamana aliyopewa na chama, siyo fursa ya kujinufaisha binafsi.
“Cheo ni dhamana. Sitakitumia chama kwa faida yangu binafsi. Nitahakikisha haki inatendeka kwa kila mgombea,” amesema Asas
Aidha amekemea tabia za baadhi ya wanachama wanaokosa nidhamu na kugeuza chama kuwa sehemu ya anasa, akisisitiza kuwa CCM inapaswa kuheshimiwa na kufuata misingi yake ya uongozi. “CCM si disco. Tunapaswa kuwa na heshima kwa chama na kufuata misingi yake”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yasin, amewataka wanachama wa chama hicho kushikamana na kuacha mivutano isiyo na tija, badala yake wajikite katika kuimarisha mshikamano na umoja ndani ya chama.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya maandalizi ya uchaguzi mkuu, alieleza kuwa serikali itahakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa vyama vyote vya siasa, akisisitiza usawa kwa wagombea wote watakaoshiriki.