Latest Posts

ASKOFU BAGONZA- DOLA INAENDESHA VYAMA VYA SIASA TANZANIA

Ikiwa ni saa chache tangu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu kutangaza kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa, wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika Alhamisi tarehe 12 Desemba 2024, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, ametoa maoni yake kuhusu jambo hilo.

Akizungumza na kituo cha habari cha SAUT Digital, Askofu Bagonza amevigusia vyama vya siasa nchini Tanzania, akisisitiza kuwa vyama hivyo vinakosa mwelekeo wa kidemokrasia na kubaki kuwa mali ya viongozi badala ya wanachama. Ameelezea changamoto zinazokumba vyama vya siasa, akisema kuwa bado kuna safari ndefu ya kuimarisha demokrasia ndani ya vyama hivyo.

Askofu Bagonza ameeleza kuwa vyama hivyo vimejikita katika kuwa mali ya viongozi huku matashi na maamuzi ya wanachama yakipuuzwa.

“Vyama vyetu vya siasa hapa nchini vina tatizo moja kubwa, ni vyama vya viongozi, si vyama vya wanachama. Matashi ya wanachama hayaheshimiwi na viongozi, na michakato ya kidemokrasia ndani ya vyama bado ina kasoro kubwa,” amesema Askofu Bagonza.

Ameongeza kuwa viongozi wanamiliki vyama huku michakato ya uongozi ikitegemea nguvu ya dola badala ya kuwa na sera za wazi na zinazojali maslahi ya wanachama.

Katika kulinganisha vyama vya siasa, Askofu Bagonza ameweka wazi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) si mfano mzuri wa demokrasia ya ndani ya vyama. Amesema kuwa viongozi wa CCM wanateuliwa kupitia mfumo wa itifaki badala ya uchaguzi wa kidemokrasia.

“Hata ndani ya CCM, huwa hawachagui Mwenyekiti. Wanamsubiri mtu anayeteuliwa kugombea urais, kisha wanamfanya mwenyekiti wao. Hii inadhihirisha kuwa CCM haifuati misingi ya demokrasia ya ndani ya chama,” amesema.

Kuhusu CHADEMA, Askofu Bagonza amezungumzia hatua ya Lissu kutangaza nia ya kugombea uenyekiti wa taifa. Amesema ni bora mtu kutangaza nia waziwazi badala ya kufanikisha mipango kwa kificho.

“Afadhali Lissu ametangaza waziwazi kuliko wale wanaogombea kwa kificho. Suala la iwapo anazo hekima za kutosha za kuongoza chama, ni jukumu la wanachama kuamua kupitia mchakato wa kidemokrasia,” amesema Bagonza.

Askofu Bagonza ameweka bayana kuwa, licha ya mfumo wa vyama vingi kufikisha miaka 30 nchini Tanzania, vyama vya siasa bado vinaendeshwa kwa ushawishi wa dola, mara nyingi kwa kificho. Amevitaja vyama kama CCM, CHADEMA, ACT, CUF, na NCCR Mageuzi kuwa bado havijakidhi matarajio ya kidemokrasia ya Watanzania.

“Vyama hivi vinaendeshwa zaidi na dola kwa wazi au kwa kificho. Hii inatuonesha kuwa tuna safari ndefu ya kuyafanya vyama viwe vya kidemokrasia,” amesema.

Aidha Askofu Bagonza amewaelekeza viongozi wa CCM na CHADEMA kutambua dhamana walizonazo katika kubeba matumaini ya Watanzania. Amesisitiza kuwa vyama hivi vinatakiwa kuwa mfano wa siasa za haki na ukweli ili kuondokana na migogoro isiyoisha.

“Vyama hivi viwili, CCM na CHADEMA, vitake visitake vimebeba msitakabali wa matumaini ya Watanzania. Tunatumaini kuwa vinatambua dhamana vilivyonayo na vitafanya siasa za haki na za kweli,” amesisitiza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!