Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, ameandika ujumbe wenye tafakuri nzito kuhusu dhana ya haki na amani, akisisitiza kuwa haki ni msingi wa amani ya kweli.
Kupitia andiko lake lililochapishwa hivi karibuni katika mitandao ya kijamii, Askofu Bagonza ametaja mambo yanayoashiria changamoto zinazokwamisha mshikamano wa kitaifa, akieleza kuwa haki inapaswa kuwa kiungo cha umoja bila kujali itikadi za kisiasa, dini, jinsia, au hali ya mtu kiuchumi.
Katika maelezo yake, Askofu Bagonza ameeleza kuwa katika mazingira ya sasa, haki imeanza kupimwa kwa misingi ya dini na si hoja inayotolewa.
“Mtu anapozungumzia haki, anatazamwa yeye ni dini gani badala ya kusikiliza anachosema. Mtu akiongelea haki, anatazamwa ni wa chama gani badala ya kusikiliza hoja yake,” ameandika.
Ameendelea kufafanua kuwa hata mtu akilalamikia kupotelewa na nduguye, badala ya kusikilizwa, anahukumiwa kuwa anavuruga amani.
“Mbuzi akipotea anapatikana, lakini mtu akipotea hapatikani. Kupoteza mtu ni kutunza amani, lakini kulalamika kuwa mtu amepotea ni kuvuruga amani,” amesema.
Askofu Bagonza ameeleza kuwa kuna udhaifu katika namna haki na amani zinavyotazamwa, akisema kuna wanaoamini kuwa amani inaweza kudumu bila haki, jambo alilolieleza kuwa haliwezekani.
“Yaonekana kuna dini inayohubiri amani bila kuhubiri haki, na kuna dini inayojifanya kuhubiri haki bila kuhubiri amani. Mimba ya haki ni amani, lakini amani bila haki ni tasa,” amesema.
Ameeleza kuwa taifa limegawanyika kati ya wale wanaoamini kuwa silaha ni chombo cha vurugu na wale wanaoamini kuwa silaha ni chombo cha kutunza amani.
“Msuluhishi wa kweli anaitwa HAKI. Tunahitaji mradi wa kimkakati wa kujenga Bwawa la Haki ya kuzalisha Amani,” ameandika Askofu Bagonza.
Katika andiko lake, Askofu Bagonza amewakumbusha viongozi kuwa wanapaswa kuzingatia kiapo chao cha utumishi kwa watu wote kwa haki bila upendeleo, akimnukuu Rais wa Tanzania ambaye aliapa kuongoza kwa haki.
“Rais ni wetu sote. Anaongoza wapenda haki na wapenda amani. Hatuna shaka na mahaba yake kwa amani. Wapenda haki wanasikia baridi. Tulimsikia akiapa kuongoza kwa haki. Bahati njema, haki ilimbeba. Akiibeba kama ilivyombeba, amani itafurika kama Bwawa la Mwalimu Nyerere,” ameandika.
Amemalizia kwa kunukuu methali ya Kijaluo inayosema: “Kuchelewa kwenda msalani, hakuzuii njaa kuuma,” akisisitiza kuwa haki haiwezi kuzuiliwa na kucheleweshwa bila kuleta madhara.