Na; mwandishi wetu
Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki Askofu Emmaus Mwamakula ameandika chapisho lake linaloeleza tafakuri aliyonayo ya Kikatiba kuhusu ukomo wa uongozi kwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa ngazi mbalimbali
Chapisho la Askofu Mwamakula alilolitoa leo, Alhamisi Desemba 19.2024 kupitia mitandao yake binafsi ya kijamii kwa kiasi kikubwa limehoji ni wakati gani hasa viongozi wa CHADEMA kuanzia ngazi za chini kabisa kufikia majimbo, wilaya, mikoa, Kanda hadi Taifa, ambapo msingi wa chapisho hilo unatokana na andiko la ‘Mwenyekiti’ wa CHADEMA mkoa wa Njombe Rose Mayemba kuonesha wasiwasi wake na mashaka kuwa huenda asishiriki mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Januari 2025 kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kwa sababu ya ‘kuahirishwa’ kwa uchaguzi wa mkoa wa Njombe siku za nyuma
“Nasikitika kuna kila dalili ya kukosa haki yangu ya kupiga kura kwenye mkutano mkuu Taifa kwa sababu ya vurugu zilizosababishwa na mgombea mwenzangu pamoja na wafuasi wake siku ya uchaguzi wa mkoa Njombe ambazo zilipelekea uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti uahirishwe” -Rose Mayemba
Andiko hilo la Rose Mayemba aliloliweka katika mitandao yake binafsi ya kijamii limeibua hisia mseto miongoni mwa wadau ambapo kila mmoja amekuwa na mtazamo wake, ambapo mmoja wa wadau hao ni Askofu Mwamakula
Ifahamike kuwa Askofu Mwamakula kwenye tafakuri yake pia ameangazia endapo Rose Mayemba na wenzake walioathiriwa na kuahirishwa kwa uchaguzi wa mkoa wa Njombe lakini walikuwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kabla ya mwaka huu (2024), Askofu huyo ameandika yafuatayo:
“Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe Rose Mayemba ameandika katika ‘twiti’ yake kuwa anaweza asiwe Mjumbe katika Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa chama unaotarajiwa kufanyika Januari 2025, ‘twiti’ yake yatufikirisha kuhusu Katiba yao juu ya ukomo wa uongozi je, Katiba ya CHADEMA inasema nini kuhusu ukomo katika ngazi ya nafasi ya Mwenyekiti na hasa ngazi ya jimbo, wilaya, mkoa na Taifa? je, ukomo wake ni siku anapotimiza miaka mitano ya kukaa madarakani tangu achaguliwe au siku ambayo utakapofanyika uchaguzi mwingine? je, kamauchaguzi ukiahirishwa au kusogezwa mbele Mwenyekiti anakoma kuwa Mwenyekiti au ataendelea kuwa Mwenyekiti hadi Uchaguzi utakapofanyika?” -Askofu Mwamakula
“Uchaguzi mkuu wa CHADEMA (wa mwisho) ulifanyika 18 Desemba 2019, hii ina maana kuwa (Desemba 18.2024) ndio ukomo wa miaka mitano (5) ya uongozi wa Mbowe (Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa), Lissu (Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara) na Wajumbe wengine wa Kamati Kuu kama tutaangalia kigezo cha kalenda, kwa hiyo kama ukomo unaangalia kigezo hicho, maana yake ni kuwa Lissu na Mbowe sio viongozi wa CHADEMA Taifa na hivyo wao sio wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Januari 2025, lakini kama ukomo huo unaangalia kigezo cha Kikatiba cha kuhitimisha uchaguzi Kikatiba, hii ina maana kuwa wao bado viongozi, Wajumbe na wapiga kura, na kama ni hivyo, Mwenyekiti wa Njombe ambaye uchaguzi wake uliahirishwa, na yeye bado ni kiongozi, Mjumbe na pia mpiga kura katika Mkutano wa Januari 2025” -Askofu Mwamakula
“Mantiki ya sheria ni kuwa uongozi unakoma Kikatiba baada ya kufanyika uchaguzi mkuu labda kama Katiba inaweka masharti ya ziada lakini kabla ya hapo uongozi wa juu na chini unabaki kuwa ni halali, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mkoa wa Njombe ambao uliahirishwa, kama viongozi wa mkoa walijiuzulu kwanza, Rose anakosa sifa ya kuwa Mjumbe na kiongozi ila kama viongozi hao hawakujiuzulu basi yeye bado ni kiongozi na mpiga kura kama walivyo Lissu na Mbowe, suala la uhalali wa ujumbe wa Mwenyekiti wa mkoa wa Njombe katika uchaguzi mkuu wa CHADEMA ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa kura ya mkoa wa Njombe ina maamuzi katika uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, nini kimekushangaza? je, nini maoni yako?” -Askofu Mwamakula