Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), katika kuadhimisha Siku ya NGOs duniani ya tarehe 27 Februari, umefanya kikao cha kimkakati na viongozi wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Dkt. John Kalage ameeleza matumaini yake kuhusu mchango wa AZAKI, akisisitiza kuwa juhudi za mashirika haya zinachangia mabadiliko chanya na endelevu ndani ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Kalage amesisitiza kuwa punguzo la ufadhili ni changamoto, lakini pia linatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya AZAKI, serikali, na sekta binafsi ili kuongeza ufanisi wa kazi zao.
Kwa upande wake, Wakili Olengurumwa amesema kuwa siku ya NGO’s Duniani, ambayo huadhimishwa tarehe 27 Februari, ni wakati wa kutafakari na kujadili masuala nyeti yanayoikabili sekta hii, yakiwemo kutokuwa na uhakika wa kifedha, kanuni kandamizi zinazoathiri ushiriki wa kidemokrasia (ikiwa ni pamoja na uchaguzi), uhitaji wa kuimarisha utekelezaji wa mapendekezo ya OECD/DAC nchini
Takwimu zinaonesha kuwa kutoka kwa jumla ya fedha zinazotolewa na wanachama 32 wa DAC, ni 7% pekee zinazowafikia AZAKI za ndani, huku 93% zikipelekwa kwa wafadhili wa nchi hizo na NGO’s za kimataifa (INGOs).
Aidha, ripoti zinaonyesha kuwa ni 25% tu ya fedha zote kutoka serikali ya Marekani kupitia USAID zinawafikia mashirika ya ndani, huku 75% zikielekezwa kwa INGOs na mashirika yaliyosajiliwa ndani ya nchi lakini yenye uhusiano wa moja kwa moja na wahisani wa nje.
Kikao hicho cha kimkakati kinalenga kuanzisha Kamati ya Kitaifa ya AZAKI kwa DAC, ambayo itakuwa na jukumu la kushirikiana na wafadhili kupitia mikutano ya mtandaoni na ya ana kwa ana, ili kuhamasisha utekelezaji bora wa Mapendekezo ya DAC nchini Tanzania.