Serikali ya Tanzania inalenga kuongeza rudisho la uwekezaji (Return on Investment – ROI) kutoka asilimia 7 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 10 ifikapo mwaka ujao wa fedha.
Dhamira hiyo imeelezwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Machi 28, 2025, wakati wa kufunga mkutano wa siku tatu wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, uliofanyika Kibaha, mkoani Pwani.
“Niwape changamoto ya kukuza rudisho la uwekezaji kutoka asilimia 7 ya sasa kwenda zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka. Na ili kufikia azma hii, mnapaswa kuongeza ufanisi wa utendaji,” amesema Balozi Kusiluka.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, serikali inasimamia jumla ya taasisi 308, ambapo 56 kati ya hizo ni kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache. Uwekezaji wa jumla ya Sh86.3 trilioni umefanywa katika taasisi hizo, huku Sh2.9 trilioni zikiwa kwenye kampuni za hisa chache, na Sh83.4 trilioni zikielekezwa kwenye taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.
Balozi Kusiluka amewataka wakurugenzi wa bodi kuongeza ufanisi ili gawio la serikali liongezeke katika mwaka ujao wa fedha.
“Ninaamini mwaka ujao wa fedha nitaona gawio kutoka taasisi mnazosimamia likiongezeka. Hiyo ni changamoto ninayowaachia,” amesema katika mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kwa mwaka wa fedha uliopita, serikali ilipokea gawio la Sh195 bilioni kutoka kampuni zake za hisa chache, kulingana na takwimu za Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Balozi Kusiluka amebainisha kuwa mafanikio haya yanaakisi juhudi za serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
Aidha, amewataka wakurugenzi wa bodi kuzingatia mwongozo ulioboreshwa wa usimamizi wa kampuni za hisa chache, uliozinduliwa Jumatano ya wiki hiyo katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.
“Nimeupitia kwa kina na nimeona umejaa miongozo mizuri itakayotusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na kwa wakati,” amesema huku akiipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuandaa mwongozo huo.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amewataka wawakilishi wa serikali kwenye bodi za kampuni za hisa chache kuhakikisha kuwa serikali inanufaika ipasavyo na uwekezaji wake.
“Nyie ni jicho la serikali, hivyo mnapaswa kutokuchukulia kiwepesi nafasi mlizopewa. Vinginevyo, mtakuwa hamuitendei haki serikali na Watanzania wote kwa ujumla,” amesema Bw. Mchechu.
Ameongeza kuwa wakurugenzi wa bodi wanapaswa kujitathmini na kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii. “Lazima mjidhatiti, na kama unaona hauko kwenye nafasi ya kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha, ni vyema ukasema ili nafasi hiyo wapewe wengine,”.