Latest Posts

BALOZI WA MAREKANI AVUNJA UKIMYA: AIKOSOA TANZANIA KWA “KUKUZA” SAKATA LA MWANAJESHI ALIYEKAMATWA NA MABOMU.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andy Lentz, ameelezea kutoridhishwa kwake na jinsi Serikali ya Tanzania na vyombo vya habari vilivyolishughulikia suala la kukamatwa kwa raia wa Marekani aliyekuwa na silaha katika mpaka wa Sirari.

Akizungumza hivi katika mahojiano maalum yaliyochapishwa na The Citizen tarehe 29 Januari, 2026, Balozi Lentz ameuita mchakato wa kuweka wazi tukio hilo kwenye vyombo vya habari kuwa ni “jambo la kusikitisha” na “lisilofaa.” Amesema kuwa suala hilo limekuzwa kupita kiasi na viongozi wa serikali, huku akisisitiza kuwa masuala ya faragha ya raia wa Marekani yanapaswa kuheshimiwa.

“Ilisikitisha sana jinsi ambavyo taarifa hiyo yote ilivyokuzwa kwenye vyombo vya habari na baadhi ya maoni yaliyotolewa na maafisa wa serikali. Kuna masuala ya faragha yanayohusu raia wa Marekani na hayo yanapaswa kuheshimiwa. Hivyo, nataka nianze na hilo kwanza kabisa. Lakini hiyo ilikuwa habari ambayo kiukweli haikupaswa kuwa habari kubwa”, ameeleza.

Sakata hilo linahusu kukamatwa kwa Charles Onkuri Ongeta (30), raia mwenye uraia pacha wa Marekani na Kenya, ambaye pia ni mwanajeshi wa Marekani mwenye cheo cha Sajenti. Ongeta alikamatwa Novemba 16, 2025, katika mpaka wa Sirari akijaribu kuingia Tanzania kutokea Kenya akiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser (KDP 502Y).

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Tarime Rorya ilibainisha kuwa Ongeta alikutwa na mabomu ya kurushwa kwa mkono aina ya CS M68. Kamanda wa Polisi alisisitiza wakati huo kuwa mabomu hayo ni silaha ambazo hata kama mtuhumiwa angeomba kibali, asingereuhusiwa kuingia nazo nchini kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Balozi Lentz amekiri kuwa ni kweli raia wa Marekani alivuka mpaka, lakini akasisitiza kuwa tukio hilo lilikuwa ni “lisilo na uzito wa kuwa habari”. Ameeleza kuwa ubalozi umefanya mazungumzo mazito na Serikali ya Tanzania kuhusu usalama na faragha za Wamarekani takriban 140,000 wanaozuru Tanzania kila mwaka kama watalii.

“Kukuza suala hadharani halikuwa jambo la kufaa,” amesema Balozi Lentz. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Marekani kuhakikisha kuwa raia wake wanapata haki zao, ikiwemo ulinzi wa faragha na msaada wa kisheria wanapokuwa kizuizini bila kudhalilishwa hadharani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!